Pata taarifa kuu
AFRIKA KUSINI

Maelfu ya watu nchini Afrika Kusini waendelea kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa kiongozi wa zamani wa taifa hilo, Nelson Mandela

Wananchi wa Afrika Kusini hii leo wanaendelea kutoa heshima zao za mwisho na kuuaga mwili wa Rais wa kwanza Mzalendo wa Taifa hilo Hayati Nelson Mandela aliyefariki dunia alhamisi ya juma lililopita jijini Johannesburg. Tayari maelfu ya waombolezaji walishiriki zoezi hilo kuanzia jana jumatano pamoja na familia ya Mandela ambao kwa pamoja na walilizunguka jeneza la wazi la kinara huyo wa ubaguzi wa rangi kuashiria kuanza rasmi kwa siku tatu za utoaji wa heshima za mwisho.

REUTERS/Marco Longari/Pool
Matangazo ya kibiashara

Bado kumekuwapo na misafara na misururu mirefu kuelekea kwenye ikulu ya nchi hiyo mjini Pretoria, ambapo mwili wa kiongozi huyo unalala hapo kwa siku tatu.

Wakati wananchi wa Afrika kusini wakiendelea kutoa heshima zao za mwisho kwa mwili wa Nelson Mandela mjini Pretoria, raia wa kigeni nao wameendelea kufurika nchini humu kutoa heshima zao kwa mwili wa Mandela huku wakimlilia wakisema aliwaunganisha na kuwapa hata uraia licha ya kuwa walitoka nje ya Afrika Kusini.

Familia ya Mandela imesema imeguswa na jinsi umati wa watu waliofika kutoa heshima ya mwisho kwa mpendwa wao, na hiyo ni ishara ya kuthamini matendo mema ambayo yalifanywa na Hayati Mandela.

Mamia kwa maelfu ya watu maarufu duniani wakiwemo Wakuu wa nchi mbalimbali walihudhuria ibada maalumu ya kumkumbuka Mandela siku ya jumanne, Rais wa Marekani Barack Obama ni miongoni mwa viongozi wa Kimataifa waliohudhuria kumbukumbu hiyo.

Mwili wa Mandela unatarajiwa kuzikwa siku ya jumapili ya tarehe 15 mwishoni mwa juma katika kijiji cha Qunu.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.