Pata taarifa kuu
UKRAINE-URUSI-Usalama

Ukraine: Mapigano yashuhudiwa Donetsk

Takribani watu 74 wameuawa na wengine 116 wamejeruhiwa katika kipindi cha siku tatu kufuatia mapigano yanayoendelea katika jimbo la Donetsk kati ya jeshi la Ukraine na waasi wanaoshikilia baadhi ya maeneo mashariki mwa Ukraine, kitengo cha afya cha utawala wa jimbo hilo kimefahamisha.

Msafara wa kijeshi karibu na jimbo la Donetsk, ambako mapigano yanaendela kushuhudiwa.
Msafara wa kijeshi karibu na jimbo la Donetsk, ambako mapigano yanaendela kushuhudiwa. REUTERS/Valentyn Ogirenko
Matangazo ya kibiashara

“Wakaazi 74 wa jimbo la Donetsk wameuawa na wengine 116 wamejeruhiwa katika kipindi cha siku 3 kutokana na mapigano”, kitengo hicho kimeongeza.

Hayo yakijiri milio ya zana nzito za kijeshi imesikika jumatano wiki hii katika mji wa Donetsk, na baadhi ya majengo ya serikali yameshambuliwa, ikiwemo chuo kikuu na makao makuu ya ofisi ya mashtaka yanayoshikiliwa na waasi. Watu wawili wameuawa katika mapigano hayo.

Jeshi la Ukraine likiendelea na mashambumbulizi dhidi ya waasi kwa lengo la kurejesha mji wa Donetsk kwenye himaya yake.
Jeshi la Ukraine likiendelea na mashambumbulizi dhidi ya waasi kwa lengo la kurejesha mji wa Donetsk kwenye himaya yake. Reuters

Kombora moja lilidondoka kwenye chuo kikuu cha ufundi, na kumjeruhi muhadhiri mmoja, huku kombora lingine likiharibu sehemu ya paa ya ofisi ya mashtaka inayoshikiliwa na waasi waliyojitenga na Ukraine, ameshuhudia mwanahabari wa shirika la habari la Ufaransa AFP.

Kwa mujibu wa duru kutoka chuo kikuu hicho cha ufundi, watu wawili, dereva na mpitanjia wameuawa katika mashambulizi hayo.

Milipuko inaendelea kusikika katikati ya mji wa Donetsk. Mtaa wa kibiashara ambako kulidondoka makombora mawili, ambayo hayajalipuka, umezingirwa na polisi. Polisi imebaini kwamba makao makuu ya polisi ndiyo yamekua yamelengwa na makombora hayo.

Manispa ya jiji la Donetsk imewataka raia kusalia nyumbani, ikiwasihi kwamba kunaweza kusikika milipuko ya hapa na pale katika maeneo mengi ya mji.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.