Pata taarifa kuu

Marekani: baada ya kulazwa hospitalini, mkuu wa Pentagon aahidi uwazi zaidi

Lloyd Austin, Waziri wa Ulinzi wa Marekani, alikiri Jumamosi Januari 6 kushindwa kuripoti kulazwa kwake hospitalini, taarifa ambayo iliwekwa wazi kwa kuchelewa, pamoja na Ikulu ya White House kulingana na vyombo vya habari kadhaa.

Lloyd Austin, Waziri wa Ulinzi wa Marekani (picha yetu ya kielelezo) alikiri, Jumamosi hii, Januari 6, kushindwa kuripoti kulazwa kwake katika hospitali ya kijeshi ya Walter-Reed tangu Januari 1, 2024.
Lloyd Austin, Waziri wa Ulinzi wa Marekani (picha yetu ya kielelezo) alikiri, Jumamosi hii, Januari 6, kushindwa kuripoti kulazwa kwake katika hospitali ya kijeshi ya Walter-Reed tangu Januari 1, 2024. AP - Cliff Owen
Matangazo ya kibiashara

Kinyume na itifaki, kulazwa hospitalini kwa Lloyd Austin, mkuu wa Pentagon tangu Jumatatu Januari 1 kwa shida za kiafya kuliwekwa wazi jioni ya Ijumaa Januari 5 na Wizara ya Ulinzi. Hili lilizua shutuma kali kutoka kwa chama cha wanahabari wa Pentagon. Alilazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi kwa siku nne, na bado alikuwa hospitalini Jumamosi, Januari 6, kulingana na NBC News. Tarehe ya kuruhusiwa kutoka hospitalini bado haijajulikana, amesema msemaji wa Wizara ya Ulinzi, akithibitisha kwamba Bw. Austin hata hivyo alikuwa ameanza tena "kazi zake" Ijumaa jioni.

"Nimejitolea kufanya vizuri zaidi"

Mshauri wa Usalama wa Kitaifa Jake Sullivan na maafisa wa Ikulu hawakufahamishwa hadi siku nne baada ya Bw Austin kulazwa hospitalini, Gazeti la kila siku la Politico limeripoti. Bwana Sullivan kisha akamuonya Rais Joe Biden, na Bunge la Marekani lilipata taarifa hiyo dakika kumi na tano kabla ya habari hiyo kuwekwa hadharani, kulingana na chanzo hicho. “Natambua kwamba ningeweza kufanya kazi nzuri zaidi ya kuhakikisha kwamba wananchi wanapewa taarifa ipasavyo. Nimejitolea kufanya vyema zaidi,” Bw. Austin alisema kutoka Hospitali ya Kijeshi ya Walter Reed karibu na Washington. "Ninachukua jukumu kamili kwa maamuzi yangu," alisisitiza katika taarifa, akibainisha kwamba "atarejea Pentagon hivi karibuni".

Rais Joe Biden na Waziri wake wa Ulinzi walizungumza Jumamosi jioni, afisa wa Ikulu ya White House ameripoti, akisisitiza kwamba mazungumzo yalikuwa "makali". “Rais ana imani kubwa na Bw. Austin. Anatazamia kurejea Pentagon,” afisa huyo ameliambia shirika la habari la AFP. Lloyd Austin alilazwa hospitalini "kwa matatizo yaliyotokea kufuatia utaratibu wa matibabu usio wa dharura," msemaji wa Pentagon Pat Ryder alisema Ijumaa jioni.

Kashfa"

Ucheleweshaji huu wa mawasiliano ya serikali umezusha ukosoaji mkubwa nchini Marekani. "Waziri wa Ulinzi ndiye kiungo muhimu katika safu ya amri kati ya rais na jeshi, pamoja na safu ya kamandi ya nyuklia, wakati maamuzi mazito zaidi yanapaswa kufanywa kwa dakika chache," alisema Jumamosi Seneta wa chama cha Republican Tom Cotton, mjumbe wa Kamati ya vikosi vya ulinzi. "Ikiwa makala hii (kutoka Gazeti la Politico) ni ya kweli, kushindwa huku kwa kushangaza lazima kuwe na matokeo," alisisitiza.

Kwa upande wake, Chama cha Waandishi wa Habari wa Pentagon kimeelezea "wasiwasi mkubwa" katika barua, kikisema kuwa kuchelewesha tangazo hilo kwa siku kadhaa hadi "jioni siku ya Ijumaa ni kashfa." "Kila wakati," Msaidizi wa Waziri wa Ulinzi Kathleen Hicks, ambaye ameidhinishwa kuchukua majukumu ya waziri ikiwa hawezi kufanya kazi, alikuwa "tayari kuchukua hatua," Pat Ryder alisema. "Alifanya maamuzi ya kawaida wiki hii kwa niaba" ya Bw. Austin, msemaji wa Pentagon baadaye ameliambia shirika la habari la AFP.

Mvutano mkali

Kulazwa hospitalini kwa mkuu wa Pentagon Lloyd Austin kunakuja katika hali ya mvutano mkali kwa Marekani nchini Ukraine, au katika Mashariki ya Kati, kuhusiana na mzozo kati ya Israel na Hamas. Waasi wa Houthi wa Yemen wanaoungwa mkono na Iran pia wameongeza mashambulizi dhidi ya meli za wafanyabiashara katika Bahari Nyekundu, huku makundi mengine nchini Iraq na Syria yakishambulia vikosi vya Marekani vilivyoko katika nchi hizo kwa usaidizi wa makombora na ndege zisizo na rubani.

(Na AFP)

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.