Pata taarifa kuu

Uchaguzi DRC: Je vifaa vya uchaguzi vitatumwa kwa wakati unaofaa nchini kote?

Zimesalia siku mbili pekee kabla ya Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi (CENI) kumaliza kusafirisha vifaa vya uchaguzi katika nchi hii kubwa iliyojaa migogoro ya kivita. Ituri, mashariki mwa nchi, ni mojawapo ya maeneo yaliyotengwa ambayo yamekumbwa na ghasia. Hata hivyo, Tume Huru ya Uchaguzi, CENI, inahakikisha hilo, kila kitu kitakuwa tayari siku ya Jumatano.

Watu 26 ambao wameidhinishwa na Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi (Céni) kuwania katika uchaguzi wa urais wa Desemba 20, 2023 nchini DRC.
Watu 26 ambao wameidhinishwa na Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi (Céni) kuwania katika uchaguzi wa urais wa Desemba 20, 2023 nchini DRC. © Studio FMM
Matangazo ya kibiashara

Kutokana na msaada wa MONUSCO, ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani, 99% ya vifaa vya uchaguzi vilipelekwa katika miji mikuu ya wilaya ya Ituri, kulingana na CENI. Ikiwa ni pamoja na miji mikuu ambayo inajikuta iko chini ya ushawishi wa wanamgambo, kama Ndjugu, Mahagi na Aru, anaripoti mwandishi wetu maalum huko Bunia, Gaëlle Laleix.

"Ni wanamgambo wa Kongo na wanamgambo hawa wana haki ya kupiga kura. Walikubali kwamba tuendelee na uandikishaji. Tulizungumza na viongozi wa jamii mbalimbali, walituruhusu kutumwa kwa vifaa kwa ajili ya uandikishaji bila hata hivyo kutokea tukio lolote baya. Na wanamgambo hawa wanakubali kwamba tupeleke vifaa kwa ajili ya kupiga kura,” anaelezea Jimmy Anga Matadri katibu mkuu wa CENI katika mkoa wa Ituri.

Hali tete magharibi mwa Ituri

Hali ni tete katika magharibi mwa mkoa wa Ituri. Maeneo matatu ya Irumu, Mambasa na Oïcha huko Kivu Kaskazini yanakabiliwa na uvamizi wa ADF, wanamgambo kutoka Uganda ambao walitangaza kuwa mshirika wa Islamic State. “Kuna tatizo kubwa katika hili. Kuna juhudi ambazo bado zinahitajika kufanywa, lakini hii iko ndani ya uwezo wa mamlaka ya kijeshi ya mkoa. Tulifuata hotuba ya gavana wa kijeshi wiki iliyopita, alihakikisha kwamba katika kanda zote, wapiga kura watapiga kura Desemba 20,” kulingana na Deogratias Bungamuzi, rais wa baraza la vijana la mkoa wa Ituri.

Hapa, kwa mujibu wa MONUSCO, zoezi la kupeleka vifaa katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Kusini, pamoja na ule wa Ituri, linaendelea. Kati ya mwezi wa Aprili na Mei, tume hii ya Umoja wa Mataifa ilisafirisha tani 128 za vifaa vya uchaguzi. Na tangu Desemba 5, kutokana na usaidizi wa MONUSCO kwa kutumia helikopta zake, tani 127 za ziada zilitumwa. Hizi ni pamoja na mashine zinazotumiwa kwa kupiga kura na kadi za kupigia kura.

Ndege za Misri

Ili kufidia ucheleweshaji huo, serikali ya Kongo, kwa upande wake, ilitangaza siku ya Jumapili kuwasili kwa ndege mbili za Hercules C-130 kutoka kwa jeshi la Misri kusaidia uwekaji wa vifaa vya uchaguzi, anaelezea mwandishi wetu huko Kinshasa, Patient Ligodi. Ndege hizi zitasaidiana na kundi linaloundwa na vyombo vingine vya usafiri vya Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FARDC) na helikopta za MONUSCO.

Ndege hizo, zilizotolewa na jeshi la Misri, zinatambuliwa na wataalamu wa serikali kwa uwezo wao mbalimbali, uimara, na pia uwezo wao uliothibitishwa wa kufanya kazi katika mazingira tofauti, iwe katika operesheni za kijeshi au za kiraia kote ulimwenguni. Sifa za ndege hizo pia zinatokana na uwezo wao wa kupaa na kutua kwenye njia fupi au hata ambazo hazijatayarishwa, ambayo inalingana na masharti ya kupelekwa katika maeneo ya mbali zaidi ya DRC.

Kulingana na baadhi ya wataalam, ndege mbili zinaweza kuwa hazitoshi, lakini serikali inahakikisha: ndege zingine za jeshi la Kongo pia zitahamasishwa. Hata hivyo, hakuna maelezo zaidi yaliyotolewa kuhusu hili. Kuhusu mikoa mingine, ujumbe wa Umoja wa Mataifa unaonyesha kuwa unaendelea kuwasiliana na CENI ili kubainisha mahitaji maalum na maeneo ya mwisho ya kupelekwa kwa vifaa vya uchaguzi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.