Pata taarifa kuu

Diplomasia: Kenya na DRC zaendelea kuvutana, Ruto azungumza

Rais wa Kenya William Ruto, amesema, Nairobi ilikataa ombi la Kinshasa, la kutaka kukamatwa kwa wanasiasa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wakiongozwa na Corneille Nangaa, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi kwa kutangaza kuundwa kwa vuguvugu jipya la kisiasa, akishirikiana na makundi ya waasi, likiwemo lile la M 23.

Rais William Ruto akiwa na mwenzake Felix Tshisekedi wakati walipokutana miezi kadhaa iliyopita jijini Kinshasa
Rais William Ruto akiwa na mwenzake Felix Tshisekedi wakati walipokutana miezi kadhaa iliyopita jijini Kinshasa AFP - ARSENE MPIANA
Matangazo ya kibiashara

Wakiwa jiji kuu la Kenya Nairobi wiki iliyopita, Nangaa akiwa pamoja na kiongozi wa kundi la M 23 Bertrand Bisimwa walitangaza kuunda vuguvugu jipya la kisiasa waliloliita Alliance Fleuve Congo, wakisema wanataka "kuikoa nchi yao".

Akizungumzia mvutano wa kidiplomasia unaendelea kati ya nchi yake na DRC, rais Ruto amesema wanasiasa hao wa DRC hawawezi kukamatwa kwa sababu ya kutumia ardhi ya Kenya kutoa tangazo hilo. Aidha, amesema, Kenya ni nchi ya kidemokrasia.

“Hatuwakamati watu kwa kutoa taarifa. Tunawakamata wahalifu,” amesema Ruto, akiongeza kuwa serikali nchini Kenya haitoi kibali kwa watu wanaotaka kuzungumza na wanahabari.

Awali, Waziri wa Mambo ya nje wa Kenya Musalia Mudavadi, alisema, Kenya haina uhusiano wowote na wanasiasa hao wa DRC na kile walichokisema katika tangazo lao.

Kitendo cha Nangaa ambaye anaishi nje ya nchi kutumia ardhi ya Kenya kutoa tangazo la kuundwa chama cha siasa na waasi, kimezua mvutano wa kidiplomasia, ambao umepelekea DRC kumrudisha nyumbani  Balozi wake kutoka jijini Nairobi  kwa mashauriano.

Wiki iliyopita, msemaji wa serikali ya DRC Patrick Muyaya, alidokeza  tangazo la Nangaa sio la kizalendo na kusema Kinshasa ilitaka maelezo ya Nairobi ni kwanini iliruhusu wapinzani hao wa serikali kutumia ardhi yake.

Haya yanajiri wakati huu DRC ikielekea kwenye uchaguzi mkuu siku ya Jumatano, lakini pia katika kipindi hiki ambacho kikosi cha Jumuiya ya Afrika Mashariki ambacho pia kinaundwa na  wanajeshi wa Kenya kikiondoka jimboni Kivu Kaskazini.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.