Pata taarifa kuu

Wanajeshi wa Sudan Kusini katika kikosi cha Afrika Mashariki nchini DRC waondoka

Zoezi la kujiondoa kwa kikosi cha Afrika Mashariki (EAC-RF) kilichotumwa mashariki mwa DRC na ambacho serikali ya Kinshasa ilikataa kuokiongezea tena muda wa kuhudumu Mashariki mwa DRC, baada ya kuona kuwa hakifanyi kazi vilivyo, limeendelea siku ya Ijumaa pamoja na kuondoka kwa askari 250 wa Sudan Kusini kutoka Goma, timu ya shirika la habari la AFP imebainisha.

Wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Sudan Kusini (SSPDF) wakijiandaa kutumwa DRC baada ya sherehe zao za kuondoka katika makao makuu ya SSPDF mjini Juba mnamo Desemba 28, 2022.
Wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Sudan Kusini (SSPDF) wakijiandaa kutumwa DRC baada ya sherehe zao za kuondoka katika makao makuu ya SSPDF mjini Juba mnamo Desemba 28, 2022. AP - Ben Curtis
Matangazo ya kibiashara

Takriban wanajeshi 300 wa Kenya kutoka katika kikosi hiki, ambao muda wao unamalizika Desemba 8, waliondoka Goma, mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini, siku ya Jumapili wiki iliyopita.

Wakiwa na uchovu, silaha mikononi, wanajeshi wa Sudan Kusini waliondoka kwenye uwanja wa ndege wa Goma mwendo wa saa 05:20 asubuhi kuelekea Juba. Kundi lingine la wanajeshi wa Sudan Kusini liliondoka baadaye asubuhi, kilibaini chanzo cha EAC-RF. Mbali na wanajeshi wa Kenya na Sudan Kusini, EAC-RF pia inajumuisha wanajeshi wa Uganda na Burundi.

Waganda na Warundi pia wanapaswa kuondoka katika wiki zijazo, kilisema chanzo hicho. Maafisa wataondoka mwisho. "Zoezi hilo litafanyika kwa kipindi cha mwezi mmoja, yaani hadi Januari 7," chanzo hicho kimeongeza. Vifaa vitaondoka kwa kutumia barabara. Wanajeshi wa Uganda na Burundi pia wapo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo chini ya makubaliano ya pande mbili na Kinshasa.

Wanajeshi wa EAC-RF walianza kuwasili Goma mnamo Novemba 2022, takriban mwaka mmoja baada ya kuibuka tena katika mkoa wa Kivu Kaskazini uasi wa M23 ambayo, kwa kusaidiwa na Rwanda kulingana na vyanzo vingi, imechukua sehemu kubwa ya jimbo hilo. Kisha mamlaka ya Kongo iliialika EAC kupeleka jeshi lake kukomboa maeneo yaliyotekwa na waasi.

Lakini Wakongo haraka wakawalaumu sana wanajeshi wa EAC, wakiwashutumu kwa kushirikiana na waasi badala ya kuwalazimisha kuweka silaha chini. Mwishoni mwa mkutano wa kilele wa EAC mnamo Novemba 25, jumuiya hii ilitangaza kwamba DRC "haitaongeza tena muda kwa jeshi hilo la kikanda ifikapo Desemba 8, 2023".

Kuchukua nafasi hiyo, Kinshasa inategemea hasa wanajeshi kutoka Jumuiya ya Kusini mwa Afrika (SADC). Msemaji wa Rais wa Kongo Félix Tshisekedi alitaja tarehe ya Desemba 10 kwa ajili ya kuanza kutumwa kwao, ambayo haijathibitishwa kwa wakati huu na SADC au na nchi wanachama wa jumuiya hii.

Kuondoka kwa EAC-RF kunakuja wakati mapigano yakiendelea kati ya M23 na jeshi la Kongo linaloungwa mkono na wanamgambo wanaoitwa "wazalendo". Ujumbe wa Umoja wa Mataifa, MONUSCO, zamani ukiitwa MONUC, umekuwepo DRC tangu mwaka 1999. Lakini pia unashutumiwa kwa uzembe na Kinshasa inaomba kuondoka kwake, "kwa utaratibu" lakini "haraka", kuanzia Januari 2024.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.