Pata taarifa kuu
USHIRIKIANO-DIPLOMASIA

Vijana wa Malawi walitumwa kwenye mashamba ya Israeli yaliyotelekezwa

Mamia kadhaa ya vijana wa Malawi wameondoka kuelekea Israel kufanya kazi kwenye mashamba yaliyotelekezwa kufuatia mashambulizi ya Hamas na milipuko ya mashambulizi ya anga ya Israel huko Gaza, serikali ya Malawi imetangaza siku ya Jumatatu.

Maelfu ya wafanyakazi wa kilimo wameondoka katika mashamba ya Israel tangu mashambulizi ya Hamas Oktoba 7.
Maelfu ya wafanyakazi wa kilimo wameondoka katika mashamba ya Israel tangu mashambulizi ya Hamas Oktoba 7. © AFP
Matangazo ya kibiashara

Ndege ya kwanza iliyobeba vijana 221 iliondoka Malawi kuelekea Israel siku ya Jumamosi, wizara ya kazi ya nchi hiyo ndogo ya kusini mwa Afrika imetangaza, ikiongeza kwamba wengine watachukua njia hiyo hiyo hivi karibuni. Maelfu ya wafanyakazi wa kilimo wameondoka katika mashamba ya Israel, sekta muhimu ya uchumi wa nchi hiyo, tangu mashambulizi ya Hamas ya Oktoba 7 ambayo yalisababisha mashambulizi makubwa ya Israel ya kulipiza kisasi dhidi ya Gaza.

Wengine walikuwa wageni na walirudi katika nchi zao. Wengine walikuwa Wapalestina kutoka Gaza ambao walinyimwa vibali vyao vya kufanya kazi Israel baada ya mashambulizi ya Hamas. Baadhi ya wafanyakazi wa kigeni ni miongoni mwa watu 239 waliochukuliwa mateka Oktoba 7 na Hamas, kulingana na Israel.

Kulingana na Waziri wa Kazi wa Malawi, Wezi Kayira, Israel ni moja ya nchi zinazolengwa na mpango wa serikali unaonuiwa kutafuta kazi kwa vijana wake nje ya nchi, na hivyo kuwezesha nchi hiyo kupokea fedha za kigeni ambazo imekuwa ikihitaji sana. Bw. Kayira amesisitiza dhamira ya serikali yake katika kuhakikisha usalama wa vijana wa Malawi wanaotumwa Israel, akihakikisha kwamba watafanya kazi katika maeneo "salama".

Kuondoka kwa vijana hao kumekuja wiki mbili tu baada ya Israel kutoa msaada wa dola milioni 60 kwa Malawi, ambayo inapambana na mgogoro wa kiuchumi. Serikali ya Malawi imekosolewa na wanaharakati wa haki za binadamu kuhusu namna mpango huo ulivyotiwa saini.

Muungano wa Watetezi wa Haki za Kibinadamu (HRDC) kwa hivyo ulilaani "usiri" unaodumishwa kuhusu makubaliano haya na serikali, na kutoa wito kwa mamlaka kuhakikisha usalama wa wafanykazi nchini Israeli. Kiongozi wa upinzani nchini Malawi, Kondwani Nankhumwa, alilaani mpango huo wiki iliyopita bungeni, na kuutaja kuwa ni wa "kishetani." "Hakuna mzazi mwenye akili timamu anayeweza kumpeleka mwanaye au binti yake katika nchi yenye vita," alisisitiza.

Malawi imeendeleza uhusiano wa karibu na Israel kwa miaka mingi, wakati nchi nyingine za Kiafrika zimetetea kwa kiasi kikubwa zaidi haki za Wapalestina. Malawi ilituma katika miaka ya nyuma wahitimu wa kilimo huko Israeli. Muda mfupi baada ya kuingia madarakani mwaka wa 2021, Rais Lazarus Chakwera alitangaza kufunguliwa kwa ubalozi wa Malawi nchini Israel mjini Jerusalem, mara ya kwanza katika miongo kadhaa kwa nchi ya Kiafrika katika mji huu wenye mzozo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.