Pata taarifa kuu

Ghasia nchini Sudan zakithiri, Umoja wa Mataifa waonya

Baada ya miezi saba ya vita na kuongezeka kwa mapigano hivi karibuni kati ya jeshi na wanamgambo wa RSF, ghasia nchini Sudan zimekithiri na kuwa "uovu mtupu", afisa wa Umoja wa Mataifa ameonya siku ya Ijumaa, akihofia hasa kuhusu mashambulizi ya kikabila huko Darfur.

Wasudan waliokimbia vita katika jimbo la Darfur nchini Sudan, wakivuka mpaka wa Sudan na Chad huko Adré, Agosti 4, 2023.
Wasudan waliokimbia vita katika jimbo la Darfur nchini Sudan, wakivuka mpaka wa Sudan na Chad huko Adré, Agosti 4, 2023. REUTERS - ZOHRA BENSEMRA
Matangazo ya kibiashara

"Tunaendelea kusema kwamba hali ni ya kutisha na ya kusikitisha. Lakini kusema ukweli, hatuna maneno ya kuelezea hali ya kutisha inayotokea Sudan," Clementine Nkweta-Salami amesema katika mkutano na waandishi wa habari.

"Tunaendelea kupokea ripoti za kutisha na za kusikitisha za unyanyasaji wa kijinsia na maovu mbalimbali, watu kupotezwa ghafla, kukamatwa na kuwekwa kizuizini kiholela na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na watoto." "Kinachotokea kinapakana na uovu kabisa," amebainisha, akimaanisha watoto "waliopatikana kwenye mapigano" au wasichana wadogo waliobakwa mbele ya mama zao.

Pia ameonyesha wasiwasi wake kuhusu "ripoti za kutatanisha za kuongezeka kwa ghasia na mashambulizi dhidi ya raia, ikiwa ni pamoja na ghasia ambazo zinaonekana kuegemea kwenye ukabila, huko Darfur." Alipoulizwa kuhusu hatari ya kurudiwa kwa mauaji ya halaiki ya mapema miaka ya 2000 katika eneo hili la magharibi mwa Sudan, amesema ana "wasiwasi sana". "Tunaendelea kutumaini kwamba hatutaishia hapo."

"Miaka 20 iliyopita, ulimwengu ulishtushwa na ukatili mbaya na ukiukwaji wa haki za binadamu huko Darfur. Tunahofia kwamba hali kama hiyo inaweza kutokea tena," amesema Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Wakimbizi, Filippo Grandi, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari. "Kumalizika mara moja kwa mapigano na pande zote kuheshimu raia pasipokuwa na masharti ni muhimu ili kuepusha janga jipya," ameongeza.

Uporaji

Kulingana na UNHCR, katika siku za hivi karibuni, "zaidi ya watu 800 wameuawa na makundi yenye silaha huko Ardamata, Darfur Magharibi, eneo ambalo hadi sasa haliathiriwi sana na vita." Ardamata pia ilikuwa inawapa hifadhi watu waliolazimika kutoroka makazi yao, ambapo karibu makazi 100 yaliharibiwa, kulingana na UNHCR. Hata hivyo, visa vingi vya uporaji - hasa wa vitu vya msaada vya shirika - vimeripotiwa katika eneo hilo.

UNHCR imesema inasikitishwa sana na ripoti za unyanyasaji wa kingono, utesaji, mauaji ya kiholela, unyang'anyi wa raia na kulenga watu wa makabila, pamoja na ripoti kwamba maelfu ya watu waliokimbia makazi yao walilazimika kukimbia kambi ya El-Geneina.

Shirika hilo linajiandaa kwa wimbi jipya la wakimbizi nchini Chad. limesema, "wale ambao wamefanikiwa kukimbia na kufaulu kuvuka mpaka wanawasili kwa wingi", akibainisha kuwa "zaidi ya watu 8,000 wamekimbilia nchi jirani ya Chad katika wiki iliyopita pekee - idadi ambayo huenda huenda iko juu kutokana na ugumu wa kujiandikisha kwa "wakimbizi wapya". 

Vita kati ya mkuu wa jeshi, Jenerali Abdel Fattah al-Burhane, na vikosi vya Msaada wa Haraka (FSR) vya Jenerali Mohamed Hamdane Dagloa ambavyo vilianza Aprili 15, vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 9,000, kulingana na makadirio ya shirika lisilo la kiserikali la Armed Conflict Location & Event Data Project (ACLED). Vita hivyo pia vimeharibu miundombinu mingi na kuwafanya zaidi ya watu milioni 4.8 kuwa wakimbizi ndani ya Sudan na milioni 1.2 katika nchi jirani, kulingana na UNHCR.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.