Pata taarifa kuu
MAZUNGUMZO-AMANI

Mazungumzo ya amani kati ya Sudan yaanza tena Jeddah

Pande zinazokinzana nchini Sudan zimeanza tena mazungumzo nchini Saudi Arabia kujaribu kumaliza vita vya miezi sita ambavyo vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 9,000, Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia imetangaza Alhamisi.

Jenerali Abdel Fattah al-Burhan (kushoto) na Jenerali Mohamed Hamdan Daglo almaarufu Hemedti (kulia), viongozi wa pande mbili zinzokinzana nchini Sudani.
Jenerali Abdel Fattah al-Burhan (kushoto) na Jenerali Mohamed Hamdan Daglo almaarufu Hemedti (kulia), viongozi wa pande mbili zinzokinzana nchini Sudani. © AP
Matangazo ya kibiashara

"Ufalme wa Saudi Arabia unakaribisha kuanzishwa tena kwa mazungumzo kati ya wawakilishi wa vikosi vya Wanajeshi wa Sudan na vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) katika mji wa Jeddah," imesema taarifa hiyo. Tangu mwezi Aprili, vita kati ya vikosi vya mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhane na makamu wake wa zamani Mohamed Hamdane Daglo, mkuu wa RSF, vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 9,000 - kulingana na idadi ndogo sana - na zaidi ya watu milioni 5.6 waliolazimika kuyatoroka makaazi yao.

Pande hizo mbili zilitangaza Jumatano kwamba zimekubali mwaliko wa kuanza tena mazungumzo huko Jeddah (magharibi), chini ya uangalizi wa Marekani na Saudi Arabia. Majaribio ya awali ya upatanishi yalisababisha mapatano ambayo yalisambaratika haraka. Wawakilishi kutoka nchi za IGAD, muungano wa Afrika Mashariki unaoundwa na Kenya, Djibouti, Ethiopia na Sudan Kusini, wanashiriki katika mazungumzo ya Jeddah kwa niaba ya Umoja wa Afrika, inasema taarifa ya Saudia kwa vyombo vya habari.

Wizara ya Saudia imetoa wito kwa wajumbe wa mazungumzo kuheshimu makubaliano ya awali yaliyotangazwa Mei 11 ya kuwalinda raia na makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyotiwa saini Mei 20. imezitaka pande zinazozozana "kukomesha umwagaji damu na kupunguza mateso ya watu wa Sudan." Riyadh pia imesema inatumai makubaliano ya kisiasa yatahakikisha "usalama, utulivu na ustawi wa Sudan na raia wake".

Usitishaji mapigano kwanza

Kabla ya kusitishwa kwa duru ya hivi punde ya mazungumzo huko Jeddah mwezi Juni, wapatanishi walikuwa wamechanganyikiwa zaidi na kusita kwa pande zote mbili kufanya kazi kuelekea suluhu ya kudumu. Kulingana na wataalamu, Jenerali Burhane na mpinzani wake Daglo wanaonekana kuchagua vita vya uasi, wakiwa na matumaini ya kupata makubaliano zaidi baadaye katika meza ya mazungumzo.

Washington imeongeza mawasiliano ili kuhakikisha kuanzishwa tena kwa mazungumzo haya na mkuu wake wa diplomasia, Antony Blinken, alikamilisha masharti wakati wa ziara yakewiki iliyopita nchini Saudi Arabia, kulingana na afisa wa Marekani. Mazungumzo hayo yanalenga kupata usitishaji vita lakini ni mapema kujadili suluhu la kudumu la kisiasa, maafisa wa Marekani wamesema.

Duru mpya ya mazungumzo italenga "kusitishwa kwa mapigano, ufikiaji usiozuiliwa wa misaada ya kibinadamu" kwa Sudan na "hatua zingine za kujenga imani", kulingana na mmoja wa maafisa hawa. Wakati mazungumzo yakianza tena Alhamisi, mashahidi wameripoti mapigano huko El Fasher, mji mkuu wa Darfur Kaskazini, na RSF imetangaza kwamba wapiganaji wake wamechukua "udhibiti kamili" wa nafasi za jeshi huko Nyala, mji mkuu wa Darfur Kusini na mji wa pili kwa idadi kubwa ya watu nchini Sudan.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.