Somaliland yapuuza mapendekezo ya rais wa Uganda kuhusu mazungumzo ya amani
Somaliland imesema haina mpango wa kufanya mazungumzo kuhusu mipango ya kujadili suala ya amani, hatua inayokuja baada ya rais wa Uganda Yoweri Museveni, kujitolea kuwa mpatanishi kati ya eneo hilo ambalo limejitenga na serikali ya shirikisho ya Somalia.
Imechapishwa:
Jumapili ya wiki iliyopita, rais Museveni, alisema amekubali kuchukua nafasi ya mratibu wa amani kati ya pande hizo mbili baada yake kukutana na mjumbe wa serikali ya Somaliland jijini Entebbe Uganda.
Wakati wa mazungumzo hayo, rais Museveni alisema haungi mkono mpango wa eneo la Somaliland kujitenga akisema halikuwa suala bora.
Katika taarifa yake, wizara ya mambo ya kigeni ya Somaliland ilisema mazungumzo ya aina yoyote na serikali ya Mogadishu, hayatajadili suala ya umoja bali yanapaswa kujadili namna pande hizo mbili zinaweza kusonga mbele kibnafsi.
Somaliland ilitangaza kuwa huru kutoka kwa Somalia mwaka wa 1991 na imekuwa ikitaka kutambuliwa kama nchi huru bila ya mafanikio.
Mazungumzo kati ya pande hizo mbili yamekuwa yakifanyika kwa miaka kadhaa sasa, suala ya uongozi wa anga, uhuru wa eneo la Somaliland yakiwa mojawapo ya mambo yanayozungumziwa.