Pata taarifa kuu

Vifo vya tetemeko la ardhi Morocco vyaongezeka na kufikia zaidi ya 2,000

Idadi ya waliofariki kwenye tetemeko la ardhi nchini Morocco imeongezeka hadi kufikia watu zaidi ya 2,000, na zaidi ya watu 1,400 wamejeruhiwa vibaya, na majeruhi wengi zaidi wako katika majimbo ya kusini mwa Marrakesh, kwa mujibu wa Wizara ya mambo ya ndani ya Morocco.

Wanajeshi wa Morocco wakindoa mwili wa mtu aliyefariki kutokana na tetemeko la ardhi, huko Tafeghaghte, Septemba 9, 2023.
Wanajeshi wa Morocco wakindoa mwili wa mtu aliyefariki kutokana na tetemeko la ardhi, huko Tafeghaghte, Septemba 9, 2023. AFP - FADEL SENNA
Matangazo ya kibiashara

Tetemeko hilo lenye ukubwa wa richa 6.8, lilitokea usiku wa kuamkia Jumamosi katika maeneo yenye milima, kwa mujibu wa watalaam.

Miji ya pwani ya Rabat, Casablanca na Essaouira imetikiswa pia na tetemeko hilo, linaloelezwa kuwa baya zaidi kuwahi kuripotiwa nchini Morocco, huku maeneo kadhaa ya nchi jirani ya Algeria pia yakitikiswa na tetemeko hilo.

Mfalme Mohammed VI alitangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa na kuamuru kupelekwa makazi, chakula na msaada mwingine kwa walionusurika.

Mtandao wa Internet umekatwa mjini Marrakesh huku umeme ukikatika baada ya tukio hilo, huku watu ambao hawajapatikana wanaoaminiwa kufunikwa kwenye vifusi vya majengo yaliyoporomoka wakitafutwa.

Nchi mbalimali zajitolea kusaidia Morocco

Waziri Mkuu wa Uingereza, Rishi Sunak amesema Uingereza ilikuwa tayari kuisaida Morocco. "Tunaungana na kila mmoja aliyeathiriwa na tetemeko mbaya la ardhi huko Morocco jana usiku.

"Uingereza iko tayari kusaidia marafiki zetu wa Morocco," alisema katika ujumbe kwenye mtandao wa X, zamani ikijulikana kama Twitter.

Wakati huo huo Shirika la misaada la Uingereza liko tayari kutuma timu ya waokoaji nchini Morocco.

Rais wa Marekani Joe Biden, akiwa nchini India anakohudhuria mkutano wa G 20 alisema amesikitishwa na maafa ya watu nchini Morocco.

“Nasikitishwa sana na kilichotokea nchini Morocco, tunawaombea,” amesema.

“Marekani iko tayari kutoa msaada unaohitajika,” amliongeza.

Rais wa China, Xi Jinping naye pia ametuma salamu za rambirambi kwa wananchi wa Morocco baada ya tukio hilo.

Viongozi wa mataifa ya Ulaya pia wamekuwa wakituma salamu za pole, huku Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu, akisema  nchi yake iko tayari kuisaidia Morocco ilirejesha uhusiano wa kidiplomasia mwaka 2020.

Mwaka 2004, watu wengine 628 walipoteza maisha na wengine 926 wakajeruhiwa baada ya tetemeko lingine kutokea katika eneo la Al Hoceima Kaskazini mwa nchi hiyo. Mwaka 1960, tetemeko lenye ukubwa wa ritcha 6.7, lilisababisha vifo vya watu 12,000 katika mji wa  Agadir.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.