Pata taarifa kuu

Viongozi wa Afrika wataka uwekezaji zaidi kwa mambo ya mabadiliko ya tabianchi

NAIROBI – Mkutano wa siku tatu, uliokuwa unajadili hali ya mazingira barani Afrika na kuwakutanisha wakuu wa nchi mbalimbali, watunga sera na wanaharakati, umemalizika leo mchana jijini Nairobi.

Rais wa Kenya William Ruto (katikati) akitoa hotuba yake ya kuhitimisha mkutano wa kwanza wa hali ya hewa barani Afrika, Mkutano wa Kilele wa Hali ya Hewa barani Afrika, jijini Nairobi Septemba 6, 2023.
Rais wa Kenya William Ruto (katikati) akitoa hotuba yake ya kuhitimisha mkutano wa kwanza wa hali ya hewa barani Afrika, Mkutano wa Kilele wa Hali ya Hewa barani Afrika, jijini Nairobi Septemba 6, 2023. AFP - LUIS TATO
Matangazo ya kibiashara

Wakuu wa mataifa 19 kwa azimio la pamoja, wamekubaliana kupaza sauti kwa Jumuiya ya Kimataifa ili kutambua uwezo wa Afrika kufanikisha nishati safi ili kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.

Mkuu wa Tume ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki, ndiye aliyesoma azimio lililokubaliwa.

Hivi karibuni Umoja wa Mataifa utaandaa mkutano wa kimataifa kuhusu hali ya hewa na COP28 itafanyika mwezi Novemba katika Umoja wa Falme za Kiarabu. Afrika, ikiwa na moyo wa Nairobi, haipaswi kwa vyovyote kukosa fursa hizi mbili za kusukuma mbele ajenda zake kuhusu hali ya hewa. Kama ilivyoombwa katika tamko hilo, pendekezo litatolewa kwa nchi wanachama kwamba mkutano wa kilele wa Afrika kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa uanzishwe kila baada ya miaka miwili.

Mwenyeji wa mkutano huo rais William Ruto, amesema azimio hilo, linaifanya Afrika kuwa na sauti moja kwenye mapambano ya tabia nchi kwenye Jukwaa la Kimataifa.

Maazimio tunayotoa hivi leo kwa ulimwengu, yanaeleza kwa wazi na kuongeza sauti msimamo wa Afrika kuhusu hatua za kuchukuliwa dhidi ya hali ya hewa, na misingi ambayo jumuiya ya kimataifa inafaa kushughulikia kuhakikisha kuwa masuala ya uchumi na ikolojia yanafanikiwa kwa ufanisi. Kuendelea mbele tutatumia kila fursa iliyopo, tukianzia na mkutano wa G20, mkutano wa Umoja wa Mataifa unaokuja ndani ya wiki mbili zijazo, mkutano wa kila mwaka wa benki ya dunia, mkutano wa IMF na pia ule wa COP28 katika kuendeleza ajenda zetu.

Katika hatua nyingine, wakati viongozi wa mataifa ya bara Afrika wakitaka mabadiliko ya mfumo wa kifedha duniani, na kuunga mkono jitahada za kupambana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kukumbatia nishati jadidifu, Ufaransa inasema mzozo kati ya mataifa tajiri na yale yanayoendelea kuhusu namna ya kukabiliana na hali hii, haupaswi kuwepo.

Chrysoula Zacharopoulou, Waziri wa Ufaransa anayehusika na masuala ya maendeleo, Francophonie na ushirikiano wa Kimataifa, alihudhuria mkutano huo ambapo ametoa kauli hii.

Hatutaki ulimwengu ambao umegawanyika, ulimwengu ni mmoja. Kile ambacho Rais Macron na rais Ruto wanajaribu kufanya pamoja ni kufanya kazi kuonesha kuwa na nia ya kisiasa, tunaweza fanya kazi kwa pamoja na kuwa na ajenda chanya. Hili ni jukumu la wanasiasa, ikimaanisha kuwa lazima tutafute suluhu kwa kizazi kipya. Kwa hivyo nafikiri tuache kuzungumzia mambo ya mgawanyiko wa kaskazini na kusini.

Ahadi ya Dola Bilioni 23 imetolewa na wadau kutoka mataifa mbalimbali, kusaidia kupambana na mabadiliko ya tabia nchi, barani Afrika.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.