Nchi za Magharibi zaahidi kusaidia mataifa ya Afrika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Mkutano wa kwanza wa ngazi ya juu wa hali ya hewa barani Afrika umeingia siku yake ya pili hii leo katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, huku wajumbe wakilenga kuweka msimamo mmoja kabla ya mikutano ijayo ya kimataifa na kujadili jinsi ya kufadhili vipaumbele vya mazingira katika bara hilo.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Rais William Ruto,mwenyeji wa mkutano huo na ambaye pia ndiye mwenyekiti wa kamati ya viongozi wa Afrika juu ya mabadiliko ya tabia nchi, amesema kuwa wakati umefika kwa Afrika kuhusishwa kikamilifu na kusikilizwa kama mmoja wa wadau wenye suluhisho.
"Ni mda viongozi wawe wazi,wakweli na waweke suluhu zote mezani ili kujiendeleza"amesema Rais William Ruto.
Wakati huo huo Ruto ametoa wito kwa vijana barani Afrika kujiweka mstari wa mbele katika kuokoa bara hili kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Kauli hii imeendana na wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliyesema kuwa vijana wakipewa fursa ya kuchangia, na kuwezeshwa kwa uwekezaji, suluhisho itapatikana kwa haraka.
Kwenye uhusiano na kongamano hilo Waziri wa Ufaransa, Chrysoula Zacharopoulou , anayeshughulika na masuala ya maendeleo ya kimataifa na Francophonie, katika ziara yake katika mtaa wa mabanda wa Mukuru ya Njenga, amesema nchi hiyo itashirikiana na mashirika mengine ya Kimataifa kusaidia kuimarisha mazingira miongoni mwa jamii masikini.
Chrysoula Zacharopoulou
Zacharopoulou , aliambatana na aliyekuwa katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban ki Moon ambaye amesema, nchi za Afrika zinapaswa kujisimamia kwenye mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi.
Ban ki Moon
Katika hatua nyingine, Ufaransa imesema itatoa msaada wa Euro millioni moja ili kuwawezesha wanafunzi kupata chakula katika mitaa duni, kama Kibera jijini Nairobi.