Pata taarifa kuu

Nafasi ya Afrika Mashariki kuandaa AFCON 2027

NAIROBI – Uchambuzi wa Jason Sagini

Nchi za Afrika Mashariki zimewasilisha ombi kwa CAF la kutaka kuanda mechi za AFCON
Nchi za Afrika Mashariki zimewasilisha ombi kwa CAF la kutaka kuanda mechi za AFCON © waziri wa michezo nchini Uganda
Matangazo ya kibiashara

Wiki iliyopita hatimaye shirikisho la soka barani Afrika (CAF) ilipokea zabuni ya pamoja kutoka kwa mataifa ya Afrika Mashariki (Kenya, Uganda na Tanzania) kutaka kuandaa kombe la mataifa ya Afrika ya mwaka 2027.

Zabuni hiyo ilipewa jina la ‘East Africa Pamoja bid’  Misri, Botswana na Algeria ni miongoni mwa waliowasilisha maombi pia. 

Nini masharti  ya kuandaa AFCON? 

Ni sharti mwanyeji awe na jumla ya viwanja sita vyenye viwango vya kimataifa ili kuchezesha timu 24. 

Aidha, lazima pia taifa liwe na viwanja vya kufanyia mazoezi kwa wachezaji na waamuzi. 

Taa za uwanja zenye uwezo wa kutumika wakati wa mechi usiku lazima ziwe katika  kila uwanja pamoja pia na paa ya uwanja kuzuia jua kali au mvua kwa mashabiki wakati wa mechi. 

Mfumo wa kidijitali wa kutoa tiketi ni muhimu sana ili kuelekeza mashabiki mlango watakaotumia na viti watakavyokaliwa kwa sababu shabiki hapaswi kuketi kwa kiti chochote kile. Hili linasaidia kudhibiti kwa haraka visa vya uhuni uwanjani. 

Mataifa ya Kenya, Uganda na Tanzania yanataka kuwa mwenyeji wa AFCON 2027
Mataifa ya Kenya, Uganda na Tanzania yanataka kuwa mwenyeji wa AFCON 2027 © State House Kenya

Nyasi za  uwanjani ni sharti ziwe laini bila milima ambayo hubabisha mpira kudunda visivyo.

Viwanja hivi ni lazima viwe na mpangilio maalum wa viti vya mashabiki, eneo la wageni mashuhuri na wanahabari pamoja pia na vyumba vya kutosha vya kubadilishia mavazi, vyoo na sehemu ya matibabu. 

Kila uwanja pia ni sharti uwe karibu na uwanja wa ndege ili kuepushia timu za taifa safari ndefu za barabarani ambazo husababisha uchovu kabla ya mechi. 

Mwenyeji pia ni lazima awe na hoteli za kutosha zenye viwango vya nyota tano ambazo zina uwezo wa kuwahudumia wageni na mashabiki kutoka bara nzima. 

Lakini je nafasi ya Afrika Mashariki kushinda haki za kuandaa ni gani ? 

Mara ya mwisho Afrika Mashariki kupata  nafasi ya kuandaa mashindano ya soka ya bara Afrika ilikuwa mwaka 2018 wakati Kenya ilipewa wajibu wa kuandaa mashindano ya CHAN ila ilifutiwa haki hizo baada ya maandalizi yake kuchelewa katika ukarabati wa viwanja.

Kwenye historia ya soka Afrika, Kombe la mataifa ya Afrika halijawahi kuandaliwa katika ardhi ya Afrika Mashariki. 

Rais wa shirikisho la soka nchini Kenya, Nick Mwendwa ni mwenye imani kubwa sana kuwa Afrika Mashariki itaandaa makala ya 2027. 

Rais wa Shirikisho la soka nchini Kenya Nick Mwendwa
Rais wa Shirikisho la soka nchini Kenya Nick Mwendwa twitter.com/nmwendwa

“Sisi tunaona ombi letu lina nguvu kuliko washindani wetu kwa sababu Algeria wameandaa CHAN mapema mwaka huu na wameandaa pia AFCON U17 mwezi huu. Misri pia iliandaa makala ya mwaka 2019,” alisema rais wa FKF Nick Mwendwa. 

“Pili, Afrika Mashariki haijawahi kuandaa AFCON nadhani CAF haiwezi kuipa Algeria na Misri mbele yetu iwapo tutaonesha kwamba tunaweza,” alisisitiza Nick Mwendwa. 

Hadi kufikia sasa, Afrika Mashariki ina uwanja mmoja tu ambao umeidhinishwa na CAF na FIFA kuandaa mechi za kimataifa – uga wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, Tanzania.  

Sehemu ya kuchezea, uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam
Sehemu ya kuchezea, uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam © tanzanianationalstadium

Kulingana na rais Nick Mwendwa, Kenya imependekeza uwanja wa kimataifa wa Moi Kasarani, Nyayo na KipKeino mjini Eldoret. Nchini Uganda, ukarabati wa uga wa Namboole ulianza baada ya CAF kupiga marufuku viwanja vyote nchini humo mapema mwaka huu.  

Kulingana na rais wa shirikisho la kandanda nchini Uganda, Peter Ogwang, uwanja huo utakuwa tayari ifikapo Juni mwaka 2023.  

Nchini Tanzania katika uwanja wa Benjamin Mkapa, katibu mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Saidi Yakubu alisema mnamo Mei 15 mwaka huu itasainiwa mikataba mitatu ya ukarabati wa uwanja huo ili kuhakikisha unakuwa bora zaidi.  

Uwanja wa Namboole nchini Uganda unaendelea kukarabatiwa
Uwanja wa Namboole nchini Uganda unaendelea kukarabatiwa © waziri wa michezo nchini Uganda

Maeneo yatakayofanyiwa ukarabati ni nyasi, vyumba vya wachezaji kubadilishia mavazi pamoja na maeneo ya kukaa wanahabari na watu mashuhuri. Tayari serikali ya Tanzania imetenga dola elfu 79 kutengeza uwanja katika maandalizi ya Afcon 2027. 

Serikali ya Kenya kupitia wizara ya michezo inayoongozwa na waziri Ababu Namwamba, ina ruwaza ya kujenga miundo misingi bora kwenye michezo zaidi ya malengo ya AFCON tu. 

Uwanja wa Kimataifa wa Moi Kasarani jijini Naiorobi nchini Kenya
Uwanja wa Kimataifa wa Moi Kasarani jijini Naiorobi nchini Kenya pbs.twimg.com/medi

“Mpango huu unaonesha tutakavyoimarisha viwanja vya Moi Kasarani na Nyayo. Kwa mfano tushaanza kuweka nambari kwenye viti katika uwanja wa Kasarani,” alisema waziri Ababu Namwamba. 

Uwanja wa Kasarani unabeba mashabiki elfu sitini ila mpangilio wa viti haujafikia viwango vya kimataifa ila kuna uwanja wa pembeni wa Kasarani Eneo maalum la kufanyia mazoezi pamoja kuwa karibu na hoteli kadhaa na uwanja wa kimataifa wa ndege wa Jomo Kenyatta. 

Uwanja wa Nyayo unahitaji kubadilishwa nyasi na kuwekwa paa pamoja na kuimarisha maeneo ya watu mashuhuri na wanahabari na vyumba vya kubadilishia. 

Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi una viti elfu  30 000.
Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi una viti elfu 30 000. Reuters

Mataifa haya matatu yana miaka miwili tu kukamilisha ukarabati wa viwanja vya jadi na ujenzi wa viwanja vingine kufikia idadi ya viwanja sita kwa pamoja.  

Hii ni kutokana na sheria za CAF kuwa wanaowasilisha maombi yao sharti wawe tayari ifikapo mwaka 2025. 

Tathmini yangu ni kuwa, CAF itaipa Afrika Mashariki haki za kuandaa AFCON 2027 si kwa kigezo kuwa wana kila kinachohitajika lakini kwa kigezo kuwa mashindano haya hayajawahi kuandaliwa Afrika Mashariki. 

Rais wa CAF, Patrice Motsepe
Rais wa CAF, Patrice Motsepe © Pierre René-Worms

Tusisahau FIFA iliipa Qatar haki za kuandaa Kombe la Dunia la mwaka 2022 licha ya kukosa uwanja hata mmoja kwa wakati huo kwa kigezo kuwa kombe hilo halijawahi kuandaliwa jangwani na walionyesha kuwa wanaweza kuandaa mashindano hayo makubwa ulimwenguni. 

Afrika Mashariki inapaswa kuiga mfano wa Qatar na kuanza kushindana na muda sababu swala la muda na kujitolea kwa serikali zote tatu kwa mtazamo wangu ndio kizuizi pekee. 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.