Pata taarifa kuu
UCHUMI-UMASIKINI

Faranga ya DRC yashuka thamani dhidi ya dola

Kushuka kwa sarafu ya DRC, malipo ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi wa umma na matumizi ya vita kumesababisha bei kuongezeka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambayo wakazi wake wanatatizika kupata bidhaa muhimu za kimsingi.

Moja ya barabara za mjini Kinshasa. Bei za usafiri, katika eneo lenye wakazi wapatao milioni 15, pia zimeongezeka.
Moja ya barabara za mjini Kinshasa. Bei za usafiri, katika eneo lenye wakazi wapatao milioni 15, pia zimeongezeka. AFP - TONY KARUMBA
Matangazo ya kibiashara

Tangu kuanza kwa mwaka huu, faranga ya Kongo imeshuka thamani kwa takriban 15% dhidi ya dola, kulingana na takwimu rasmi na wafanyabiashara wa sarafu, na hali mbaya inawakumba maskini zaidi. Faranga za Kongo elfu mbili zimekuwa zinabadilishwa hivi majuzi kwa dola 1. Kiwango kilipanda hadi zaidi ya faranga 2,320 kwa dola 1, kulingana na takwimu za hivi punde kutoka benki kuu.

Watu kadhaa waliohojiwa na shirika la habari la AFP wanasema kwamba katika baadhi ya matukio bei zimepanda zaidi, zikiongezeka maradufu au hata zaidi. Akiwa amesimama kwenye matope ya soko katika mji mkuu wa Kinshasa, Bibiche Musabili akitengeneza majani ya viazi vitamu, chakula kikuu cha kienyeji kinachotumika katika kitoweo, kiitwacho "matembele", ameelezea hali hiyo na kushindwa kupata wateja kutokana na dola kuzidi kupanda.

"Hapo awali, tulinunua shada hili la mboga kwa faranga 500 za Kongo (dola 0.25)," anasema mama mmoja. "Leo zimekuwa faranga 3,000 (dola 1.5) "Tutafanya nini?" analalamika mama wa familia, akisema kwamba watoto wake wanasumbuliwa na njaa.

Nchini DRC, theluthi mbili ya takriban wakazi milioni 100 wanaishi chini ya mstari wa umaskini, uliowekwa kuwa dola 2.15 kwa siku na Benki ya Dunia.

Shirika la Fedha la Kimataifa IMF lilisema mwezi Februari kwamba DRC iliongeza matumizi yake mwaka 2022, ili kupambana na waasi wa M23 ambao waliteka maeneo makubwa mashariki mwa nchi hiyo, lakini pia kulipa malimbikizo ya mishahara kwa watumishi wa umma.

Mfumuko wa bei ulikuwa tayari umefikia 13% mwishoni mwa mwaka jana, kwa sehemu kutokana na kuzorota kwa uchumi kutokana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Ongezeko la matumizi ya fedha mwishoni mwa 2022 lilisababisha kufurika kwa faranga za Kongo kwenye soko na mahitaji makubwa ya dola, anachambua mwanauchumi, ambaye hakupendelea kutajwa jina.

DRC, nchi kubwa katika Afrika ya Kati, dola zinakubaliwa kila mahali, katika mikahawa na maduka, na hutumiwa kwa ununuzi mkubwa zaidi.

Mchumi huyo pia anaeleza kuwa matumizi makubwa ya serikali yanalingana na uagizaji bidhaa kutoka nje ambao pengine unahusishwa na mzozo wa Mashariki na pia malipo ya malimbikizo ya mishahara.

Malipo haya yakifanywa kwa faranga za Kongo, yalisababisha msongamano wa watu kutaka kubadilisha fedha zao za ndani kwa dola. "Benki hazikuweza kutoa dola za kutosha, hivyo kushuka kwa thamani," anaongeza mtaalam huyu.

Serikali imeahidi kuchukua hatua ili kuleta utulivu wa sarafu hiyo, lakini kushuka kwa thamani ya Faranga tayari kumezua hasira. Wakati wa maandamano ya hivi karibuni ya upinzani katika mji mkuu, washiriki waliinua mabango kupinga bei ya mkate.

Bei za usafiri, katika eneo lenye wakazi wapatao milioni 15, pia zimeongezeka. Akisubiri teksi ya pamoja katikati mwa jiji, Herdi Lomboto, 19, mwanafunzi kitivo cha usimamizi, anasema hivi karibuni alilipa faranga 500 ($0.25) ili kufika nyumbani. Sasa ni kati ya faranga 1,500 na 2,000 (kati ya takriban dola 0.75 na 1).

"Inauma, anasema, kuona wazazi wetu wanaoteseka" kwa kulipa ada ya shule, usafiri na kila kitu.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.