Pata taarifa kuu

Chad yaadhimisha mwaka mmoja wa kifo cha rais mbabe wa kivita Idriss Déby

Wananchi wa Chad wanaadhimisha mwaka mmoja kamili, tangu kuuawa kwa aliyekuwa rais wao Idriss Déby Itno, wakati alipokuwa katika uwanja wa vita kupambana na waasi. 

Mkutano na waandishi wa habari wa Rais wa Chad Idriss Déby, Februari 2008 huko Ndjemena.
Mkutano na waandishi wa habari wa Rais wa Chad Idriss Déby, Februari 2008 huko Ndjemena. © AP - Jerome Delay
Matangazo ya kibiashara

Akilihutubia taifa, rais wa serikali ya mpito Jenerali Mahamat Idriss Déby Itno, ambaye ni mtoto wa rais huyo wa zamani, amesema uongozi wa mpito umesaidia nchi hiyo ya Afrika ya Kati kusalia thabiti. 

 

 

Mwezi ujao, serikali ya mpito imeandaa mazungumzo ya maridhiano, ambayo upinzani umetishia kutoshiriki. 

 

Mfahamu rais mbabe wa kivita

 

Idriss Déby, rais wa Chad kwa miaka 30, alikuwa ni mpambanaji.

Aliingia madarakani kwa mtutu wa bunduki na alitoka kwa mtutu wa bunduki.

 

Rais huyo mwenye umri wa miaka 68, ambaye alikuwa amechaguliwa kuliongoza taifa lake kwa muhula wa sita aliuawa vitani na waasi, na kuandikisha ukomo wa mtawala ambaye alisifika kwa uwezo wake vitani.

Alipokea mafunzo ya kijeshi nchini Ufaransa na kufuzu kama rubani wa ndege za kivita. Alirudi kutoka Ufaransa mnamo Februari 1979 na kukuta Chad imekuwa uwanja wa vita kwa makundi mengi yenye silaha. Déby alijiunga na wapiganaji wa Hissène Habré, mmoja wa wakuu wa wapiganaji nchini Chad. Mwaka mmoja baada ya Habré kuwa rais mnamo 1982, Déby alifanywa kamanda mkuu wa jeshi.

Alijijengea sifa mnamo 1984 kwa kuharibu vikosi vinavyoiunga mkono Libya mashariki mwa Chad. Mnamo 1985, Habré alimtuma Paris kufanya mafunzo huko École de Guerre; aliporudi mnamo 1986, alifanywa mshauri mkuu wa jeshi kwa ofisi ya rais. Mnamo 1987, alikabiliana na vikosi vya Libya uwanjani, akisaidiwa na Ufaransa katika kile kinachoitwa "Vita vya Toyota", akitumia mbinu ambazo zilisababisha hasara kubwa kwa vikosi vya maadui.

Déby apata msaada kutoka kwa Gaddafi

Uhasama hata hivyo uliibuka mnamo Aprili 1989 kati ya Habré na Déby juu ya nguvu iliyoongezeka ya kikosi cha Walinzi wa Rais. Kulingana na Human Rights Watch, Habré alipatikana na hatia ya "mauaji ya kisiasa yaliyotokana na mateso, na maelfu ya watu kukamatwa kiholela", pamoja na mauaji ya kikabila wakati ilipogundulika kuwa viongozi wa makundi mbali mbali wanaweza kuwa tishio kwa utawala wake, pamoja na wengi wa kabila la Zaghawa la Déby ambao waliunga mkono serikali.

Habré alimtuhumu Déby, waziri wa mambo ya ndani Mahamat Itno, na kamanda mkuu wa jeshi la Chad Hassan Djamous kwa kuandaa mapinduzi. Déby alikimbilia kwanza Darfur, kisha Libya, ambapo alikaribishwa na Gaddafi huko Tripoli. Itno na Djamous walikamatwa na kuuawa.

Kiongozi wa Libya wakati huo, Kanali Muammar Gaddafi - alikuwa adui mkubwa wa Habré - na alimsaidia Déby kuanzisha uasi kwa malipo ya taarifa juu ya operesheni za CIA nchini Chad.

Déby na wafuasi wake waliuteka mji mkuu wa N'Djamena mwezi Disemba 1990 - hata hivyo alikabiliana na mlima wa changamoto pamoja majaribio lukuki ya mapinduzi ya kijeshi katika miaka 30 iliyopita.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.