Pata taarifa kuu
DRC-SIASA-USALAMA

Sintofahamu yaendelea DRC siku tatu kabla ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi

Siku tatu kabla ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi nchini DRC, hali ya wasiwasi imeendelea kujitokeza huku mitambo ya radio ya kimataifa RFI ikizimwa. Hali hii inajitokeza siku mbili baada ya serikali kuchukua uamuzi wa kufunga huduma ya intaneti nchi nzima.

Mji wa Kinshasa, mji mkuu wa DRC.
Mji wa Kinshasa, mji mkuu wa DRC. © CC 2.0/MONUSCO/Myriam Asmani
Matangazo ya kibiashara

Wakati huo huo mwandishi wa Habari wa RFI Florence Morice mjini Kinshasa, amenyang'anywa kibali kinachomruhusu kufanya kazi nchini DRC. Serikali ya DRC inamshtumu mwandishi wa habari wa RFI kwamba alijaribu kurusha baadhi ya matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanyika siku ya Jumapili Desemba 30. Madai ambayo RFI imefutilia mbali na kuomba hatua hiyo ifutwe mara moja.

Radio France Internationale inakumbusha kwamba inaheshimu na iliheshimu hatua iliyochukuliwa na mamlaka nchini DRC ya kutotangaza matokeo ya uchaguzi kabla ya muda uliyowekwa na Tume ya Uchaguzi.

RFI inabaini kwamba itarusha matokeo ya Uchaguzi Mkuu ambayo yatakuwa yametangazwa na Tume ya Uchaguzi (CENI) kulingana na sheria.

Uongozi wa RFI unasema unasikitishwa na uamuzi wa kuzima mitambo yake nchini DRC tangu siku ya Jumanne wiki hii. Mitambo ya RFI katika miji ya Kinshasa, Goma, Bukavu, Kisangani, Lubumbashi, Mbandaka, Matadi na Mbuji Mayi, yote imezimwa.

Wanasiasa mbalimbali nchini DRC na wanaharakati wa mashirika ya kiraia wamekosoa hatua hiyo ya serikali ya DRC.

Kwa upande wa Jean-Pierre Bemba, makamu wa zamani wa rais wa DRC na kiongozi wa muungano wa upinzani Lamuka amesema, ikiwa RFI imezimiwa mitambo, ni kwa sababu imefanya kazi yake.

Hatua hiyo ya serikali ya DRC dhidi ya RFI imekosolewa vikali na shirika la Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka (RSF).

RSF inaona kuwa hatua hiyo ni ukandamizaji wa uhuru wa vyombo vya habari unaoendelea nchini DRC.

Matokeo ya uchaguzi nchini DRC yanatarajiwa kutangazwa Jumapili Januari 6, 2019.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.