Pata taarifa kuu
AU-MAREKANI

Umoja wa Afrika wamtaka rais Trump kuomba radhi kwa kuwadharau Waafrika

Umoja wa Afrika unamtaka rais wa Marekani Donald Trump kuomba radhi baada ya kutoa matamshi ya kibaguzi dhidi ya mataifa ya Afrika.

Rais wa Marekani Donald Trump
Rais wa Marekani Donald Trump REUTERS/Carlos Barria
Matangazo ya kibiashara

Uongozi wa Umoja wa Afrika umesema umesikitishwa sana na kushtushwa na matamashi ya Trump.

Kiongozi huyo wa Marekani alinukuliwa akiuliza ni kwanini wahamiaji kutoka mataifa ya Afrika aliyoyafananisha kama shimo la kutupa taka, wanaendelea kuja Marekani.

Ofisi ya Mwenyekiti wa Tume ya Afrika inayoongozwa na Moussa Faki Mahamat, imesema matamshi ya Trump yanawadharau watu wa Afrika pamoja na utu.

Aidha, Umoja huo unataka kuwepo kwa mazungumzo ya haraka na ya wazi kati ya Marekani na mataifa ya Afrika.

Taifa la Haiti pia limeguswa katika matamshi hayo ya rais Trump na kuyashtumu.

Botswana imemwita balozi wa Marekani nchini humo kufafanua matamshi hayo ya Trump.

Naye rais wa Senegal Macky Sall, amesema kauli ya Trump haikubaliki kamwe na kusisitiza kuwa Wafrikia wana haki ya kuheshimiwa.

Aidha, amemwagiza Balozi wa Marekani kueleza ni kwanini rais Trump alitoa matamshi hayo.

Tume ya Umoja wa Mataifa nayoshughulikia haki za binadamu pia imelaani matamshi ya Trump na kuyaita ya kibaguzi na ya aibu.

Hata hivyo, Trump kupitia ukurasa wake wa Twitter amekanusha kutoa matamshi hayo wiki hii alipokutana na wabunge, kujadili suala la wahamiaji.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.