Pata taarifa kuu
DRC-SIASA

Milio ya risasi yasikika jijini Kinshasa na Lubumbashi nchini DRC

Milio ya risasi imesikika Jumanne hii jijini Kinshasa na mji wa pili wa ukubwa wa Lumbumbashi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wakati huu polisi na wanajeshi wakipiga doria katika miji hiyo mikubwa baada ya muhula wa kikatiba wa rais Joseph Kabila kumalizika Jumatatu usiku.

Baadhi ya vijana wakiwa wamechoma matairi kwenye moja ya barabara za Kinshasa
Baadhi ya vijana wakiwa wamechoma matairi kwenye moja ya barabara za Kinshasa https://cdn-images
Matangazo ya kibiashara

Maandamano yalianza kushuhudiwa usiku wa kuamkia siku ya Jumanne katika miji hiyo huku maafisa wa usalama wakijaribu kuwazuia kwenda barabarani.

Mwandishi wa Shirika la Habari la Ufaransa AFP mjini Lubumbashi, amesema polisi wamekabiliana na waandamanaji katika mtaa wa Matuba ambapo polisi wameshuhudiwa wakifwatua risasi hewani kuwatawanya waandamanaji.

Mjini Goma Mashariki mwa nchi hiyo, kwa siku ya pili mfululizo, waandamanaji wameonekana wakiteketeza moto matairi ya magari na kukabiliana na polisi.

Kwa siku ya pili leo, shughuli zimekwama katika miji mikuu nchini humo kwa hofu ya kuzuka kwa vurugu ya kisiasa.

Kiongozi Mkuu wa upinzani  Etienne Tshisekedi  akiwataka wananchi kujitokeza kuandamana
Kiongozi Mkuu wa upinzani Etienne Tshisekedi akiwataka wananchi kujitokeza kuandamana

Wakati hayo yakijiri, kiongozi mkuu wa upinzani Etienne Tshisekedi amewataka raia wa nchi hiyo na nchi za kigeni kutomtambua rais Kabila baada ya muhula wake kufikia mwisho.

Tshisekedi mwenye umri wa miaka 84, akizungumza kupitia mkanda wa video, amewataka wafuasi wa upinzani kujitokeza na kuandamana kwa amani kumpinga rais Kabila.

Hata hivyo, raia wengi wa DRC hawakufanikiwa kuuangalia mkanda huo wa video baada ya serikali kufunga mtandao wa Internet.

Hadi sasa, hakuna dalili ya rais Kabila kuachia madaraka kwa sababu Mahakama ya Kikatiba iliamua kuwa anaweza kuendelea kuongoza hadi pale rais mpya atakapochaguliwa.

Mazungumzo ya kisiasa kati ya wanasiasa wa upinzani na wale wa serikali chini ya Kanisa Katoliki, yanatarajiwa kurejelewa hapo kesho.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.