Pata taarifa kuu
DRC-TANZANIA

DRC: upinzani wasisitiza Kabila kuondoka madarakani, mwenyewe asema yuko tayari

Muungano wa vyama vya upinzani wa “Rassemblement” umeitaka serikali ya DRC kuheshimu Katiba na kuzingatia azimio namba 2277 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Rais wa DRC, Josephu Kabila, na rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli - Dar es Salaam, Tanzania, 4 October 2016.
Rais wa DRC, Josephu Kabila, na rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli - Dar es Salaam, Tanzania, 4 October 2016. Ikulu/Tanzania
Matangazo ya kibiashara

Akizungumza wakati wa kutamatisha mkutano mkubwa wa Muungano huo, mpinzani mkongwe nchini humo Etienne Tshisekedi amesema kuwa maandamano yaliyofanyika tarehe 19 mwezi uliopita mjini Kinshasa ilikuwa kumpa rais Joseph Kabila kadi ya njano, na kusema kuwa wanajiandaa kumpa kadi nyekundu ifikapo tarehe 19 desemba mwaka huu.

Baraza la maaskofu wa kanisa katoliki, CENCO, kwa upande wake limetoa wito wa kufanyika kwa mazungumzo yanayoshirikisha pande zote, na kuwataka wanasiasa kudumisha amani, kama alivyosema kaimu katibu mkuu wa CENCO Donatien Shole.

Mkutano huu wa muungano wa upinzani umefanyika ikiwa zimepita siku chache tu toka kushuhudiwa kwa vurugu kubwa katika jiji la Kinshasa, ambapo polisi walikabiliana na waandamanaji wa upinzani waliokuwa wakishinikiza rais Kabila aondoke madarakani.

Etienne Tshisekedi, kinara wa upinzani nchini DRC.
Etienne Tshisekedi, kinara wa upinzani nchini DRC. RFI / Sonia Rolley

Hata hivyo mwishoni mwa juma, tume ya taifa ya uchaguzi nchini DRC ilipendekeza kusogezwa mbele kwa uchaguzi mkuu wa nchi hiyo uliokuwa umepangwa kufanyika mwezi ujao, na sasa ENI inataka uchaguzi huyo ufanyike mwezi November mwaka 2018, pendekezo ambalo vyama vingi vya upinzani vinapinga.

Akiwa jijini Dar es Salaam kwa ziara ya kikazi, rais Josephu Kabila Kabange, amesema serikali yake itafanya uchaguzi lakini sio kwa shinikizo la kisiasa kwa kuwa ni lazima wananchi wote wa Kongo wapate haki ya kuandikishwa kupiga kura.

Rais Kabila ameongeza kuwa yeye hana nia ya kung’ang’ania madaraka lakini anataka nchi hiyo ifanye uchaguzi uliokuwa wa huru na haki, na ndio maana aliitisha na kuanzisha mazungumzo ya kitaifa yanayofanyika jijini Kinshasa.

Kwa upande wake Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, ameunga mkono wazo la rais Kabila, ambapo nae ametaka kwanza wananchi waandikishwe ili kila mwenye umri wa kupiga kura kwenye uchaguzi ujao apate haki hiyo kwakuwa idadi imeongezeka maradufu, ambapo pia ameahidi kutuma ujumbe wa mawaziri kutoka nchi za SADC, kwenda DRC kutathmini hali ilivyo.

Katiba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Haimruhusu Rais Joseph Kabila kugombea tena kiti hicho kwa muhula wa tatu.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.