Pata taarifa kuu
UN

Wakimbizi, mgogoro wa Syria, Sudan, DRC na Burundi ni ajenda kubwa ya mkutano wa baraza la UN

Viongozi wa dunia wamekusanyika jijini New York, Marekani, tayari kwa kuanza kushiriki mkutano wa 71 wa baraza la umoja wa Mataifa, huku masuala ya wakimbizi, wahamiaji, vita na mgogoro wa Syria yakiwa ni masuala mtambuka yanayogubika mkutano wa mwaka huu.

Moja ya mikutano ya baraza la umoja wa Mataifa, mkutano wa mwaka huu umegubikwa na masuala ya vita nchini Syria pamoja na wakimbizi
Moja ya mikutano ya baraza la umoja wa Mataifa, mkutano wa mwaka huu umegubikwa na masuala ya vita nchini Syria pamoja na wakimbizi UN Photo/Manuel Elias
Matangazo ya kibiashara

Wakuu hao wa dunia wanakutana huku vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria vikiwa vimesababisha vifo vya watu zaidi ya laki 2, huku wengine zaidi ya milioni tisa wakilazimika kukimbia nchi yao kutokana na vita.

Kuenea kwa makundi ya kiislamu yenye msimamo mkali na mfululizo wa mashambulizi ya kigaidi kwenye nchi mbalimbali duniani, ni suala jingine ambalo wakuu wa dunia watajaribu kulizungumza na kutazama namna bora ya kukabiliana na tishio hili.

Suala la wahamiaji na wakimbizi kutoka nchini Syria, Libya na maeneo mengine ya bara za Afrika, ni ajenda nyingine ambayo wakuu hawa wa nchi wataizungumzia kujaribu kutatua kero hiyo, ambayo baadhi ya nchi za umoja wa Ulaya zimeanza kutofautiana kuhusu namna bora ya kushughulikia janga hili.

Nchini Ujerumani, chama tawala cha Kansela Angela Merkel, kimeshindwa vibaya kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa, kutokana na Sera yake ya kuruhusu kuingia kwa mamia ya wahamiaji ambao wamepewa kibali cha kuishi nchini humo.

Mzozo wa nchi ya Sudan Kusini, uliochangiwa na tofauti kati ya Rais Salva Kiir na aliyekuwa makamu wake wa kwanza wa Rais Riek Machar, ni suala jingine ambalo linatarajiwa kuwa kitovu cha mazungumzo yao, huku wakuu hao wa dunia wakikosolewa kutokana na kushindwa kumaliza machafuko kwenye taifa hilo.

Mzozo wa kisiasa nchini Burundi na vita dhidi ya makundi ya waasi mashariki mwa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, ni suala jingine ambalo mataifa yenye ushawishi kwa nchi hizo, yanatarajiwa kukutana na kulizungumzia kwa kina kuona ni namna gani wanaweza kutatua kero zinazoshuhudiwa hivi sasa.

Masuala mengine ambayo kwa umuhimu pia yatazungumziwa, ni pamoja na kupambana na umasikini hasa kwa nchi zinazoendelea, mapambano dhidi ya magonjwa sugu na uchangishaji wa fedha za dhalura pale zinapohitajika kukabiliana na majanga ya kibinadamu.

Hotuba ya Rais wa Marekani, Barack Obama ndio inayosubiriwa kwa hamu, kwakuwa itakuwa pia ni hotuba yake ya mwisho kwenye umoja wa Mataifa.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.