Pata taarifa kuu
DRC-SIASA

Mazungumzo ya DRC kuendelea juma hili baada ya kusimama mwishoni mwa juma

Mazungumzo ya kitaifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, yanaendelea tena juma hili, baada ya kusimama kwa siku mbili mwishoni mwa juma kupisha baadhi ya wadau wanaoshiriki mazungumzo hayo, kwenda kuzungumza na upande wa muungano wa Dynamique uliosusia mazungumzo haya.

Mpatanishi wa mzozo wa kisiasa nchini DRC, Edem Kodjo (katikati), oicha ya mwishoni mwa juma wakati wa mazungumzo hayo kabla ya kusitishwa kwa siku mbili.
Mpatanishi wa mzozo wa kisiasa nchini DRC, Edem Kodjo (katikati), oicha ya mwishoni mwa juma wakati wa mazungumzo hayo kabla ya kusitishwa kwa siku mbili. Reuters
Matangazo ya kibiashara

Mazungumzo yalisitishwa kwa siku mbili mwishoni mwa juma kufuatia ombi la kinara mwingine wa upinzani Vital Kamerhe aliyekubali kushiriki mazungumzo hayo na kujikuta akitengwa na muungano wa vyama vya upinzani unaoongozwa na kinara wa chama cha UDPS, Etienne Tshisekedi.

Akiambatana na wajumbe wengine wanaoshiriki kwenye mazungumzo hayo, Vital Kamerhe alijikuta yeye na ujumbe wake wakifungiwa milango walipofika kwenye ofisi za muungano wa Dynamique na hata kwa chama cha UDPS, ambapo aliambia hana nafasi ya kukutana na viongozi wa juu wa chama hicho.

Taarifa za watu wa karibu wa Kamerhe zinasema kuwa, kiongozi huyo alijikuta juhudi zake za kutaka kuwashawishi wanasiasa waliosusia mazungumzo zinagonga ukuta na kuambulia patupu baada ya kuambiwa kuwa ni msaliti wa harakati za demokrasia kwenye taifa hilo.

Mmoja wa waandamanaji raia wa DRC walioandamana hivi karibuni kupinga Serikali.
Mmoja wa waandamanaji raia wa DRC walioandamana hivi karibuni kupinga Serikali. DR

Juhudi za Kamerhe zilipewa nguvu na Rais wa Congo Brazzaville, Denis Sassoungueso, ambaye alifanikiwa kukutana na viongozi wa muungano wa upinzani lakini mazungumzo yake na viongozi hao nayo yaligonga ukuta kwani msimamo wao ulikuwa palepale.

Muungano wa upinzani unaoongozwa na mwanasiasa mkongwe nchini humo Tshisekedi, umeendelea kushikilia msimamo wake kuwa utashiriki mazungumzo hayo, ikiwa masharti yao yatasikilizwa na Serikali.

Upinzani unataka kuachiwa huru kwa wafungwa wote wa kisiasa pamoja na kuandaliwa kwa mazingira mazuri ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu nchini DRC.

Mazungumzo haya yalianza juma lililopita bila ya uwepo wa vyama muhimu vya upinzani pamoja na mashirika ya kiraia ambayo yaliungana na upinzani kushinikiza baadhi ya madai yao kutekelezwa kabla ya kushiriki.

Mpatanishi wa mazungumzo ya kisiasa nchini DRC, Edem Kodjo.
Mpatanishi wa mazungumzo ya kisiasa nchini DRC, Edem Kodjo. Photo MONUSCO/Theophane Kinda

Mpatanishi wa mazungumzo hayo, waziri mkuu wa zamani wa Togo, Edem Kodjo anaendelea kukutana na upinzani huku shinikizo la kutakiwa kujiondoa kama mpatanishi kwenye mazungumzo hayo likizidi kuongezeka.

Akizingumza wakati wa ufunguzi wa mazungumzo hayo, Kodjo, alisema amekuja nchini humo sio kwa matakwa ya upande au kundi lolote la kisiasa, na kusisitiza kuwa jukumu lake kama mpatanishi ni kuhakikisha mazungumzo hayo yanafanyika kwa usawa kwa kuzingatia masuala ambayo yako mezani kwa sasa.

Mazungumzo haya yanafanyika wakati huu, nchi ya DRC ikijiandaa kufanya uchaguzi wake mkuu mwaka huu, huku Rais Josephu Kabila akitakiwa kuwa ameondoka madarakani mpaka ifikapo December 19 mwaka huu, lakini kuna kila dalili kuwa uchaguzi huenda usifanyike kwa muda uliopangwa.

Tarehe 19 ya mwezi huu kwa mujibu wa katiba ya DRC, tume ya uchaguzi CENI, ina[aswa kutangaza tarehe za kuanza kwa kampeni za Urais kuelekea uchaguzi mkuu, siku ambayo upinzani uanoongozwa na Tshisekedi umesema utafanya maandamano makubwa nje ya ofisi za tume ya uchaguzi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.