Pata taarifa kuu
NIGERIA-INEC-UCHAGUZI-SIASA

Rais mteule wa Nigeria Muhammadu Buhari asema nchi yake imekua kidemokrasia

Rais mteule wa Nigeria Muhammadu Buhari amezungumza kwa mara ya kwanza na kusema ushindi wake umedhihirisha kuwa nchi yake imekua kidemokrasia.

Rais mteule wa Nigeria Muhammadu Buhari
Rais mteule wa Nigeria Muhammadu Buhari REUTERS
Matangazo ya kibiashara

Akizungumza katika makao makuu ya chama chake cha APC jijini Abuja, Buhari amemsifu rais anayeondoka madarakani Goodluck Jonathan kwa kuwa mshindani wa kipekee aliyekubali kuachia madaraka kwa amani.

Jenerali Buhari alimshinda Jonathan kwa kupata kura Milioni 15 nukta 4 dhidi ya mpinzani wake aliyepata kura ya Milioni 13 nukta3.

Wachambuzi wa siasa na waangalizi wa mambo wanasema uchaguzi huo ulikuwa huru na haki licha ya kuwepo kwa ripoti za wizi wa kura katika baadhi ya vituo na hitilafu wakati wa kupiga kura.

Buhari aliyepeperusha bendera ya chama cha APC anakuwa kiongozi wa kwanza wa upinzani kushinda uchaguzi nchini Nigeria tangu mwaka 1999.

“Tumeidhihirishia dunia kwamba sisi tumekua kidemokrasia, tumeachana na siasa za chama kimoja,” Alisema.

Aliongeza kuwa “ Nyinyi Wanaigeria, mmeshinda,”.

” Mlipigia kura mabadiliko, na mabadiliko yamekuja,” alisisitiza huku akishangiliwa na wafuasi wake.

Siku ya Jumatano, rais anayeondoka madarakani Jonathan alimpigia siku rais mteule na kumpongeza kwa ushindi huo.

Jonathan alituma taarifa kwa vyombo vya Habari na kusema “ Niliiahidi nchi kuwa kutakuwa na uchaguzi huru na haki. Nimetekeleza ahadi yangu.”

Wafuasi wa Buhari jijini Abuja
Wafuasi wa Buhari jijini Abuja AFP PHOTO / STRINGER

Habari muhimu kuhusu Muhammadu Buhari
 

  • Miaka 72
  • Muislamu kutoka Kaskazini mwa Nigeria
  • Alichaguliwa baada ya uchaguzi wa Machi 28 mwaka 2015
  • Kiongozi wa kijeshi kati ya mwaka 1984 hadi 1985
  • Aliondolewa uongozini kijeshi
  • Rekodi mbaya ya haki za binadamu
  • Anaonekana kama mtu asiyependa ufisadi
  • Mpenda nidhamu, na kuhimiza wafanyakazi kufanya bidii
  • Aliponea shambulizi dhidi ya kundi la Boko Haram

Wafuasi wa Buhari wakifurahia ushindi
Wafuasi wa Buhari wakifurahia ushindi AFP PHOTO/PIUS UTOMI EKPEI

Wafuasi wa Muhammadu Buhari wana matumaini kutokana ushujaa wa Buhari katika miaka iliyopita alipokua akihudumu katika jeshi la nchi hii na hasa kuwa anafahamu hali halisi ya taifa la Nigeria.

Wengi wanaona kuwa Buhari ataweza kukomesha ukatili unaotekelezwa na wanamgambo wa kiislamu kwa kipindi cha miaka sita sasa.

Wakaazi wa mji wa Lagos ambao ni wazaliwa wa eneo la Kaskazini mwa Nigeria wamemuomba rais mpya wa nchi ya Nigeria kujikita na ujenzi wa shule, hospitali na kuboresha miundombinu kama barabara.

Raia wengi wamempigia kura Mahammadu Buhari kutokana na rushwa ambayo imekithiri katika nchi hii yenye watu wengi barani Afrika.

Buhari ataapishwa mwisho wa mwezi ujao wa Mei.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.