Urusi yatekeleza mashambulio makubwa nchini Ukraine
Jeshi la Urusi limeishambulia Ukraine kwa kurusha makombora 122 na kutumia ndege zisizo na rubani 36 kurusha mabomu katika maeneo mbalimbali na kusababisha vifo vya watu 18.
Imechapishwa:
Mashambulio ya Ijumaa, yameelezwa kuwa makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika vita kati ya nchi hizo mbili, ambavyo vimedumu kwa miezi 22 sasa.
Jiji la Kiev limeshuhudia mashambulio yenye nguvu, na kuacha moshi mzito mweusi angani, katika maeneo yaliyoshambuliwa na jeshi la Urusi.
Mbali na Kiev, miongoni mwa miji mingine sita iliyoshambuliwa ni pamoja na Lviv , Odesa na Zaporizhzhia Kusini huku majengo yakiangushwa zikiwemo hospitali.
Hatua hii ya Urusi imekuja baada ya mapema wiki hii, jeshi la Ukraine kushambulia na kuharibu manuari ya kivita ya Urusi kwenye bandari ya Bahari nyeusi kwenye jimbo la Crimea.
Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na nchi za Magharibi zikiongozwa na Ufaransa yamelaani hatua hiyo ya Urusi, huku rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, akisema nchi yake imeshambuliwa na vifaa karibu vyote ya kivita.
Aidha, Zelensky ameyataka mataifa ya Magharibi kuendelea kuiunga mkono kwa kuipa fedha na vifaa vya kijeshi, baada ya Marekani wiki hii kutoa msaada wake wa kifedha wiki hii.