Pata taarifa kuu

Mediterania: Wahamiaji 41 hawajulikani walipo baada ya boti lao kuzama karibu na Lampedusa

Ajali nyingine ya boti lililokuwa limebeba wahamiaji kuzama imeripotiwa katika Bahari ya Mediterania, karibu na Lampedusa. Kulingana na maelezo ya watu wanne walionusurika, watu wasiopungua arobaini hawajulikani walipo baada ya boti hilo kuzama. Boti lao lililokuwa likitokea nchini Tunisia limezama wakati likielekea pwani ya Italia.

Wahamiaji wakisafiri kwa boti kusini mwa Bahari ya Mediterania karibu na Lampedusa mnamo Agosti 11, 2022.
Wahamiaji wakisafiri kwa boti kusini mwa Bahari ya Mediterania karibu na Lampedusa mnamo Agosti 11, 2022. © Francisco Seco / AP
Matangazo ya kibiashara

Boti hilo limezama kwenye Mfereji wa Sicily. Walikuwa wameondoka asubuhi, Alhamisi Agosti 3, kutoka Sfax nchini Tunisia, kwa boti iliotengenezwa kwa chuma. Walipokuwa wakielekea ufuo wa Lampedusa, umbali wa kilomita mia moja, bahari iliyochafuka sana ilipindua boti hilo saa sita tu baada ya kuondoka kwao, anaripoti mwandishi wetu huko Roma, Blandine Hugonnet.

Watoto watatu ni miongoni mwa wahamiaji hao waliokuwa wakisafiri kwenye boti hilo kuelekea Ulaya. Angalau 41 kati yao walitoweka baharini siku hiyo. Vyovyote vile, hivi ndivyo manusura wanavyosema, wakinukuliwa katika taarifa kwa vyombo vya habari na shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi (UNHCR), shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia watoto (UNICEF) na shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji (IOM). Watu wanne miongoni mwa wahamiaji hao ndio walionusurika. 

Ongezeko kubwa la idadi ya wahamiaji wanaowasili nchini Italia

Wakiokolewa na walinzi wa pwani ya Italia, manusura hawa, wanaume watatu na mwanamke mmoja kutoka Côte d'Ivoire na Guinea, waliwasili nchini Italia Jumatano hii, Agosti 9 asubuhi. Walifika Lampedusa, walitunzwa na Shirika la Msalaba Mwekundu katika kituo cha usajili cha kisiwa kidogo cha Italia.

Baada ya ajali nyingine tatu za meli katika eneo la kati la Mediterania katika siku za hivi karibuni, ni janga lingine kwenye milango ya Ulaya ambalo linaongeza idadi ya watu zaidi ya 1,800 ambao tayari wameangamia tangu mwezi Januari katika ajali ya boti katikati mwa Bahari ya Mediterania, njia iliyo mbaya zaidi ya wahamiaji duniani, kulingana na takwimu zilizokusanywa na Umoja wa Mataifa.

Takriban wahamiaji 94,000 wamewasili katika ufuo wa Italia tangu mwanzo wa mwaka, ikiwa ni zaidi ya mara mbili ya idadi hiyo kwa kipindi kama hicho mwaka 2022, kulingana na takwimu zilizotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Italia.

(Pamoja na AFP)

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.