Pata taarifa kuu

Makumi ya watu wafariki nchini Uturuki na Syria kufuatia tetemeko la ardhi

Tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 7.8 katika kipimo cha Richter limepiga kusini mwa Uturuki na nchi jirani ya Syria leo Jumatatu, na kuua karibu watu 100 katika nchi zote mbili na kusababisha uharibifu mkubwa, kulingana na ripoti za awali.

Watu wakipita karibu na vifusi vya jengo huko Pazarcik kusini mwa Uturuki mnamo Februari 6, 2023.
Watu wakipita karibu na vifusi vya jengo huko Pazarcik kusini mwa Uturuki mnamo Februari 6, 2023. AP
Matangazo ya kibiashara

Takriban watu 42 wameuawa katika miji kadhaa nchini Syria, kulingana na vyombo vya habari vya serikali, na angalau 53 nchini Uturuki kulingana na hesabu ya shirika la habari la AFP likinukuu vyanzo rasmi. Kulingana na taasisi ya Marekani inayohusika na mitetemeko ya ardhi (USGS), tetemeko la ardhi limetokea saa 04:17 alfajiri saa za Syria (sawa na saa Tisa na dakika 17 usiku sa za Afrika ya Kati), katika kina cha takriban kilomita 17.9.

Kwa mujibu wa shirika serikali la Syria SANA, ambalo linamnukuu afisa kutoka Wizara ya Afya, watu 42 waliofariki na wengine zaidi ya 200 wamejeruhiwa wamerekodiwa katika miji ya Aleppo, Hama na Latakia na huenda idadi hiyo ikaongezeka.

Kitovu hicho kinapatikana katika wilaya ya Pazarcik, katika mkoa wa Kahramanmaras (kusini-mashariki), takriban kilomita 60 kutoka mpaka wa Syria. Tetemeko hili la ardhi ni kubwa zaidi nchini Uturuki tangu tetemeko la ardhi la Agosti 17, 1999, ambalo lilisababisha vifo vya watu 17,000, ikiwa ni pamoja na maelfu huko Istanbul.

Takriban watu 23 wamefariki na wengine 420 kujeruhiwa katika jimbo la Malatya, gavana wa mkoa huo ameliambia shirika la utangazaji la TRT. Gavana wa mkoa wa Sanliurfa, aliyenukuliwa na shirika la serikali ANADULU, aliripoti vifo vya watu 17 na 30 kujeruhiwa katika mkoa wake. Takriban wengine sita wamefariki katika mkoa wa Diyarbakir, gavana wa mkoa huo amesema.

Watu wamenaswa chini ya vifusi

Kulingana na AFAD, shirika la serikali la kudhibiti majanga, tetemeko la ardhi lililotokea usiku wa manane lilikuwa na ukubwa wa 7.4 na kina cha kilomita 7. Mitetemeko hiyo, iliyosikika kusini mashariki mwa nchi, pia ilisikika huko Lebanon na Cyprus, kulingana na waandishi wa shirika la habari la AFP. Video zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha majengo yaliyoharibiwa katika miji kadhaa kusini-mashariki mwa nchi.

Mwandishi wa shirika la habari la AFP huko Diyarbakir, mji mkubwa ulioko kusini-mashariki mwa nchi hiyo, aliona jengo lililoporomoka, huku waokoaji wakiwa kazini wakijaribu kuwatoa watu kutoka kwenye vifusi. Katika Twitter, watumiaji wa mtandao wa Kituruki walishiriki utambulisho na eneo la watu waliokwama chini ya vifusi katika miji kadhaa kusini-mashariki mwa nchi.

Meya wa jiji la Adana Zeydan Karalar amesema majengo mawili ya ghorofa 17 na 14 yaliharibiwa, kulingana na TRT. Majengo yaliharibiwa katika miji mingi ya kusini-mashariki mwa nchi, ikiwa ni pamoja na Adiyaman, Diyarbakir na Malatya, kulingana na kituo cha kibinafsi cha Kituruki NTV, na kuongeza hofu ya waathirika.

(Pamoja na AFP)

 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.