Pata taarifa kuu
UFARANSA-SIASA

Ufaransa: Chama cha Rais Macron chapata wingi wa viti bungeni

Chama cha rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron hatimaye kimepata wingi wa viti ilivyohitaji bungeni baada ya kutamatika kwa uchaguzi wa duru ya pili siku ya Jumapili, Juni 18 licha ya kuwa hakikupata ushindi wa kishindo kama ilivyotarajiwa awali.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wakati alipopiga kura kwenye uchaguzi wa duru ya pili, Juni 18, 2017
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wakati alipopiga kura kwenye uchaguzi wa duru ya pili, Juni 18, 2017 June 18, 2017. REUTERS/Christophe Archambault/Pool
Matangazo ya kibiashara

Chama cha Macron chenye mwaka mmoja tu pamoja na washirika wake kilipata viti 351 katika bunge lenye viti 577, matokeo rasmi yameonesha huku kikiwaangusha baadhi ya wanasiasa wakongwe nchini humo.

Chama cha Macron kilichoundwa miezi 16 uiliyopita kimeanza kutengeneza ramani mpya ya siasa za nchi hiyo licha ya kuwa idadi ya viti imekuwa chini kuliko ilivyotarajiwa awali kuwa kingepata viti 470.

Hata hivyo idadi hii ya viti ilivyovipata bado inampa uongozi wa jumla kwenye bunge la nchi hiyo, hatua ambayo itamrahisishia kazi katika kupitisha sera zake bungeni.

Waziri mkuu Edouard Philippe amesema kuwa “mwaka mmoja uliopita hakuna aliyeamini kuwa maajabu haya yangetokea.”

Upande wa chama cha Socialist ambacho kilikuwa madarakani katika kipindi cha miaka 5 iliyopita sambamba na washirika wake kimepata kati ya viti 41 na 49, ikiwa ni idadi ndogo zaidi kuwahi kushuhudiwa.

Kiongozi wa chama hicho Jean-Claude Cambadélis ametangaza kujiuzulu nafasi yake akiwataka wanasiasa wa mrengo wa kushoto kubadili kila kitu kuanzia kwenye itikadi zake mpaka kwenye ngazi ya utawala.

Kiongozi wa chama chenye msimamo mkali cha FN Marin Le Pen yeye kwa mara ya kwanza alifanikiwa kupata kiti cha ubunge ambapo pia chama chake kimeshinda viti 8.

Le Pen amesema kuwa rais Macron anaweza kuwa amepata idadi ya viti anavyotaka bungeni, lakini “anapaswa kujua kuwa mawazo yake sio mawazo ya jumla ya nchi nzima na kwamba wananchi hawataunga mkono sera zake zitakazoidumaza nchi hiyo.”

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.