Uingereza yapiga kura ya kujitoa katika Umoja wa Ulaya
Vyombo vya Habari nchini Uingereza vinatabiri kuwa, raia wa Uingereza wamepiga kura ya kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Matokeo ya kura hiyo ya maoni iliyopigwa Alhamisi wiki hii, kuamua ikiwa nchi hiyo isalie au ijiondoe kwenye Umoja huo yanaendelea kutolewa na imetabiriwa kuwa waliopiga kura ya kujiondoa watashinda kwa asilimia 52 huku waliopiga ya kusalia katika Umoja huo wakipata asilimia 48.
Matokeo haya yamesababisha mtikisiko mkubwa kwenye soko la fedha duniani na pauni ya Uingereza imeshuka sana thamani kiwango ambacho mara ya mwisho kilishuhudiwa mwaka 1985.
Scotland na jiji la London, ripoti zinasema walipiga kura kwa wingi kusalia kwenye Umoja wa Ulaya.
Mmoja wa viongozi wa upinzani ambaye amekuwa katika mstari wa mbele kutaka Uingereza kujiondoa kwenye Umoja huo, Nigel Farage, amesema ushindi huu ni kama Uhuru kwa Uingereza.
Watu Milioni 30 walijitokeza kupiga kura, sawa na asilimia 71 nukta 8.
Wachambuzi wa uchumi duniani, wanasema ni siku ngumu sana kwa Uingereza kiuchumi lakini pia kwa Umoja wa Ulaya.
Inatarajiwa kuwa nchi hiyo itayumba kiuchumi baada ya uamuzi huu wa kuondoka kwenye Umoja wa Ulaya.