Pata taarifa kuu
AFCON 2023

Ghana, Nigeria na Misri zaanza kwa kujikwaa michuano ya AFCON 2023

Abidjan, Cote D'Ivoire – Jumapili jioni, ilikuwa siku ya matokeo mseto baada ya mabingwa wa zamani Misri, Nigeria na Ghana kupata wakati mgumu katika mechi zao za ufunguzi katika uwanja wa Olympic d’Ebimpe na Felix Houphouet Boigny jijini Abidjan.

Wachezaji wa Ghana katika mechi dhidi ya Cape Verde mnamo 14/01/2024
Wachezaji wa Ghana katika mechi dhidi ya Cape Verde mnamo 14/01/2024 © CAF
Matangazo ya kibiashara

Mapema mchana, Ivan Salvador wa Equatorial Guinea aliweka taifa lake kifua mbele dakika ya 36 dhidi ya Nigeria katika uwanja wa Olympic d’Ebimpe. Ila dakika mbili baadaye The Super Eagles wakarudisha bao hilo kupitia mshambuliaji wa Napoli na mchezaji bora barani Afrika mwaka 2023, Victor Osimhen kufuatia krosi ya Ademola Lookman iliyounganishwa wavuni kwa kichwa na Osimhen.

Katika uwanja wa Felix Houphouet Boigny, mabingwa mara saba Misri walifungua kampeni yao ya kusaka taji la nane vizuri baada ya kupata bao la mapema dakika ya kwanza kupitia shuti la mshambuliaji Mostafa Mohammed ndani ya kijisanduku.

Msumbiji ilionesha nia ya kweli ya kusawazisha kipindi chote cha kwanza ila wakaelekea mapumziko wakiwa nyuma bao 1-0.

Ari waliokuwa nayo kipindi cha kwanza, ilidhihirika wazi kufuatia msururu wa mashambulizi yaliyozalisha goli la kusawazisha kupitia kichwa chake Witiness Ouembo dakika ya 55. Dakika tatu baadaye, nguvu mpya Clesio Bauque aliwaweka kifua mbele The Mambas baadaya kupenya katikati ya beki Hamdi Mohamed na kiungo Mohammed Elneny kisha kuvurumisha shuti upande wa kushoto wa golikipa El Shenawy.

Mshambuliaji wa Misri Mostafa Mohammed (17) akifunga bao la kwanza mchezo dhidi ya Msumbiji
Mshambuliaji wa Misri Mostafa Mohammed (17) akifunga bao la kwanza mchezo dhidi ya Msumbiji © CAF

Msumbiji ilidhibiti mchezo vizuri kwa dakika zote kipindi cha pili hadi dakika ya nyongeza wakati mwamuzi Dahana Beida kutoka Mauritania alihitaji mfumo wa VAR kuhakiki mpira wa adhabu ndani ya kijisanduku, uliozalisha penalti dhidi ya Msumbiji.

Mshambuliaji wa Liverpool Mohammed Salah bila wasiwasi akawasaidia mafarao kupata pointi moja.

Kiungo wa Msumbiji Ricardo Martins alitajwa mchezaji bora wa mechi.

Baada ya mechi kocha wa Misri, Rui Vitoria alisema:

Hatukuwa na umakini wa kutosha ndio maana tulipoteza nafasi nyingi. Tunahitaji umakinifu zaidi. Najua lengo la timu ni kushinda mechi nyingi. Kwa michezo ijayo tuko tayari kupambana tena.

Kocha wa Msumbiji, Francisco Conde alisifia timu yake kwa kuendelea kuboreka huku akilenga matokeo mazuri zaidi katika mechi zijazo.

Majonzi ya Ghana

Kocha wa Ghana, Chris Hughton hakusita kuonesha huzuni yake baada ya kupoteza mabao 2-1 dhidi ya Cape Verde.

Tumesikitishwa sana tena sana na matokeo haya, na najua wachezaji pia wanajua hilo. Ni jukumu letu sasa kujiamsha na tunajua mechi yetu dhidi ya Misri ni sharti tupate matokeo ya kuridhisha.

Cape Verde ilijiweka kifua mbele dakika ya 17 kupitia kiungo Jamiro Monteiro aliyemalizia shuti la straika Jovane Cabral lililopanguliwa na mlinda lango Richard Ofori.

Dakika tisa baadaye, Ghana walifikiri wamesawazisha mechi ila mwamuzi wa kati kutoka DRC Jean Jacques Ndala Ngambo akakataa bao la kiungo Majeed Ashimeru, baada ya kuhakiki kwenye kiwambo cha VAR kuwa straika Ransford Konigsdorffer alimziba golikipa wa Cape Verde, Vozinha kuona vizuri wakati wa shuti hilo kali kutoka nje ya kijisanduku.

Hatimaye, mabingwa hao mara nne walipata bao dakika ya 55 kufuatia mpira wa kona uliochongwa na Jordan Ayew kisha ukaunganishwa wavuni na beki Alexander Djiku ambaye alitajwa mchezaji bora baada ya mechi.

Makosa ya mabeki na ukosefu wa mawasiliano sahihi katika mlango wa Ghana yalisababisha mkanganyiko ambao Cape Verde ilitumia kupata bao la ushindi dakika ya 90, kiungo Garry Rodrigues akifunga bao rahisi baada ya mlinda lango Ofori kutoka langoni kujaribu kurekebisha makosa ila alikosa kuufikia mpira.

Timu ya taifa ya Cape Verde baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya Ghana uwanjani Felix Houphouet Boigny, Abidjan 14/01/2024
Timu ya taifa ya Cape Verde baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya Ghana uwanjani Felix Houphouet Boigny, Abidjan 14/01/2024 © CAF

Kocha wa Cape Verde, Pedro Britto Bubista baada ya mechi alikuwa mwingi wa furaha.

Sisi ni nchi ndogo hivyo basi tunataka kuonesha tunaweza kupambana na timu yoyote. Ina maana kubwa sana kuipiga Ghana sababu wao ndio walitubandua kwenye mashindano yetu ya AFCON ya kwanza kushiriki mwaka 2013.

Mara ya mwisho Ghana kushinda mechi ya Kombe la Mataifa ya Afrika ni kwenye makala ya mwaka 2019 nchini Misri walipoilaza Guinea Bissau 2-0.

Ratiba ya leo:

Senegal vs Gambia, 5pm (Charles Konan Banny, Yamoussoukro)

Cameroon vs Guinea, 8pm (Charles Konan Banny, Yamoussoukro)

Algeria vs Angola, 11pm (Stade de la Paix, Bouaké)

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.