Pata taarifa kuu
CECAFA U18

Uganda yaishinda Kenya kunyakua ubingwa wa CECAFA U18 ya wavulana

Mambo Leo Stadium, Kisumu – Timu ya taifa ya Uganda ya wavulana walio chini ya miaka 18 ilitoka nyuma na kuipiga Kenya mabao 2-1 kutwaa ubingwa wa kombe la Baraza la Mashirikisho za mpira wa miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) katika uwanja wa Jomo Kenyatta Mambo Leo jijini Kisumu nchini Kenya.

Timu ya Uganda wakisherehekea ushindi wa ubingwa wa CECAFA U18 tarehe 08/12/2023
Timu ya Uganda wakisherehekea ushindi wa ubingwa wa CECAFA U18 tarehe 08/12/2023 © FUFA
Matangazo ya kibiashara

Uganda iliandaa mashindano ya CECAFA U15 mwezi Novemba na kushindwa kutwaa ubingwa huo baada ya kupoteza fainali dhidi ya Zanzibar magoli 4-3 katika mikwaju ya penalti kufuatia sare ya 1-1 kwenye muda wa kawaida.

Hakim Mutebi alifunga bao la ushindi sekunde hamsini baada ya kipindi cha kwanza kuanza katika muda wa ziada. Beki wa Kenya Collins Ochieng alishindwa kumkabili winga Alex Yiga ambaye alileta krosi kali langoni iliyowatatiza mabeki wa Kenya.

Kiungo wa Uganda Hakim Mutebi (20) baada ya kufunga bao la ushindi dhidi ya Kenya
Kiungo wa Uganda Hakim Mutebi (20) baada ya kufunga bao la ushindi dhidi ya Kenya © FUFA

Uganda ilisawazisha mchezo katika dakika ya 78 kupitia mchezaji Abasi Kheyune baada ya beki wa Kenya Amos Wanjala kukosa mawasiliano sahihi na wenzake. Mpira huo wa kona ulimpata mshambuliaji Abasi ambaye hakua amekabwa na beki yeyote.

Kenya ilitangulia kufunga kupitia mshambuliaji Syphas Awuor dakika ya 65 baada ya kuandaliwa pasi na mlinda lango Ibrahim Wanzala, pasi ndefu ambayo beki Louis Anguti alishindwa kuondoa.

Kenya ingelipata bao la pili dakika kumi baadaye, baada ya Aldrine Kibet, Tyrone Kariuki na Syphas Awuor kubadilishana pasi za haraka ila Kibet akapiga shuti nje ya lango kutumia mguu wa kushoto.

Wachezaji wa Kenya wakisherehekea baada ya kupata bao la kuongoza mchezo
Wachezaji wa Kenya wakisherehekea baada ya kupata bao la kuongoza mchezo © CECAFA

Kipindi cha kwanza kilitawaliwa pakubwa na Kenya, nafasi kubwa ya pekee kwa Uganda ikijitokeza dakika ya 19. Krosi yake Hakim Mutebi iliunganishwa vizuri na Alex Yiga lakini mabeki wa Kenya wakazuia vizuri Amos Wanjala akiondoa mpira nje kuzalisha kona ya Uganda.

Nafasi bora zaidi kwa Kenya kipindi cha kwanza ilitokea dakika ya 15, kiungo Humphrey Aroko aliupata mpira nje ya kijisanduku lakini akashindwa kufunga nafasi ya uso kwa uso na mlinda lango Abdu Magada.

Uganda walifikiri wamepata bao la kuongoza mechi dakika ya 45 baada ya winga Richard Okello kufunga bao ila mwamuzi msaidizi Renovat Bizumuremyi kutoka Burundi aliinua kibendera chake kwani Okello alikua ameotea.

'Uchambuzi wa Kimbinu'

Kocha wa Uganda, Morley Byekwaso alisema walijua Kenya si timu rahisi na walifahamu kiungo chao cha kati ndio eneo lenye nguvu zaidi.

Tunashukuru Mungu sana mpango wetu wa kwanza uliweza kufanikiwa na tukashinda. Pongezi kubwa kwa wachezaji wangu.

Kenya ililazimika kufanya mabadiliko kwenye kiungo cha kati katika kipindi cha kwanza. Kocha Salim Babu aliwatoa Joseph Khisa na Humprey Aroko na kuwaleta Aldrine Kibet na Lucas Maina.

Mshambuliaji wa Uganda, Denis Kisiriko (16) dhidi ya mabeki wa Kenya
Mshambuliaji wa Uganda, Denis Kisiriko (16) dhidi ya mabeki wa Kenya © FUFA

Kocha wa Kenya Anthony Akhulia baada ya mechi alikiri kulemewa na mabadiliko waliyofanya Uganda kwenye kipindi cha pili.

Waliwaleta wachezaji wakomavu zaidi na wenye miili mikubwa na hapo ndio walitulemea lakini nawapa pongezi kwa kushinda ubingwa. Tunaendelea kujifunza, tutarekebisha na tutafanya vyema katika mashindano yajayo.

“Tulipoteza umakini kwenye mchezo baada ya kufunga bao na mabadiliko yao yalileta presha ambayo tulishindwa kudhibiti. Huu sio mwisho ila ndio mwanzo na tutaendelea kupambana,” mshambuliaji Louis Ingavi aliiambia RFI Kiswahili.

Kocha Akhulia alitupilia mbali sababu ya kukosa kudhibiti shinikizo ya mashabiki wa nyumbani kushinda ubingwa akisisitiza Uganda waliwazidi tu kimbinu uwanjani.

Mashindano huwa magumu unapoendelea kupiga hatua kuelekea fainali. Mpira hua hivo.

Tanzania nafasi ya tatu

Mapema asubuhi, Tanzania iliridhia medali ya shaba baada ya kuishinda Rwanda mabao 3-1 katika uwanja uo huo.

“Nawashukuru wachezaji wangu kwa jinsi walivyocheza. Tulifeli kwenye nusu fainali lakini nashukuru wachezaji wangu walifuata maagizo. Niwapoa pongezi wachezaji kwa kufuata elekezo na tumemaliza vizuri,” alisema kocha Habibu Kondo.

Magoli ya Tanzania yalifungwa na Zidane Sereri, Said Said na John Misheto Rwanda ikipata bao lake kupitia Didier Ndaishimiye.

Tumejifunza mambo mengi. Tumekutana na makocha tofauti na ushindani tofauti.

Wachezaji wa Tanzania wakisherehekea baada ya kufunga bao la tatu dhidi ya Rwanda
Wachezaji wa Tanzania wakisherehekea baada ya kufunga bao la tatu dhidi ya Rwanda © TFF

Nahodha msaidizi wa Tanzania Omar Yahya alisema anafurahia kushiriki mashindano kama haya na lengo la wachezaji ni kufika mbali.

Kocha wa Rwanda Jean Baptista hakuridhika na nafasi ya nne ila alisema wataendelea kujituma zaidi kufanikiwa kwenye mashindano yajayo.

Sijafurahia  jinsi tumecheza kwenye mashindano yote. Wakati mwingi tumekua chini kutokana na kukosa ujasiri na motisha lakini vijana walijituma kwa kunisikiliza. Tungali na kazi mingi ya kufanya tufikie viwango vya Tanzania au timu ambazo zimefika fainali.

‘Waliotia Fora’

  • Mchezaji Bora - Hakim Mutebi (Uganda/SC Villa)
  • Mfungaji Bora – Aldrine Kibet (Kenya/ Nastic Sports Academy ya nchini Uhispania)
  • Kipa Bora – Ibrahim Baraza Wanzala (Kenya/Kakamega Homeboyz FC)
  • Tuzo ya Fair Play – Tanzania
  • Medali ya dhahabu - Uganda
  • Medali ya fedha - Kenya
  • Medali ya shaba - Tanzania

Sherehe za tuzo hizo zilipambwa na Waziri wa Masuala ya Vijana, Michezo na Sanaa nchini Kenya, Ababu Namwamba kama mgeni rasmi.

Wajumbe wengine waliohudhuria ni pamoja na Rais wa CECAFA, Wallace Karia, Rais wa Shirikisho la Soka nchini Kenya Nick Mwendwa na Makamu wake Doris Petra, Rais wa Chama cha Soka Sudan Kusini Augustino Maduot Parek na mjumbe wa shirikisho la soka nchini Uganda Rogers Byamukama.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.