Sahabo raia wa Rwanda kuondoka Lille ya Ufaransa
NAIROBI – Na Paulo Nzioki
Imechapishwa:
Mchezaji wa kimataifa wa Rwanda, Hakim Sahabo ameiaga klabu ya Ufaransa LOSC Lille akitajwa kuhamia Standard Liege ya Ubelgiji.
Standard Liege inayoshiriki katika ligi kuu nchini Ubelgiji Timu Jupiler Pro League inatajwa kuwa karibu kukamilisha mazungumzo ya kumsajili kiungo huyo mwenye umri wa miaka 17 na amewashukuru Lille kwa jukwaa walilompa.
"Wakati umefika wa mimi kukuaga. Asante sana kwa msaada wako usioyumba!" Sahabo aliandika katika mitandao yake ya kijamii.
Sahabo alijiunga na Lille mnamo 2021 kutoka akademia ya KV Mechelen na kucheza katika timu ya U17 kabla ya kupandishwa kwenye timu ya U19 mnamo 2022.
Alifunga mabao matano katika msimu uliomalizika hivi punde huku Lille ikimaliza ya tano kwenye jedwali la Ligi ya Championnat ya U19.
Kinda huyo mwenye kasi ya ajabu anatarajiwa kuja Kigali Juni 16 kuisaidia timu ya taifa kuelekea mechi ya kufuzu AFCON dhidi ya Msumbiji Juni 18 kwenye Uwanja wa Huye.