Pata taarifa kuu
Michezo Afrika

Ni mikakati ipi bora ya kuimarisha Soka barani Afrika

Nairobi – Panaponyesha huvimbikwa hata kwa makuti. Bara la Afrika limejaa talanta chungu nzima lakini swali ni je, talanta hizi zimefichwa wapi na viwango vya soka ya Afrika kibiashara vimesimama wapi?

Mchezaji wa zamani wa Kenya, Boniface Ambani (kushoto), mwakilishi wa FIFA Anthony Baffoe (katikati) na mkurugenzi mtendaji wa Football Foundation Africa Brian Wesaala.
Mchezaji wa zamani wa Kenya, Boniface Ambani (kushoto), mwakilishi wa FIFA Anthony Baffoe (katikati) na mkurugenzi mtendaji wa Football Foundation Africa Brian Wesaala. © rfi Kiswahili
Matangazo ya kibiashara
03:59

Biashara na mchezo wa soka

Shirika la Football Foundation for Africa linaloongozwa na Brian Wesaala liliandaa kongamano la kwanza kabisa la kibiashara juma lililopita jijini Nairobi kujribu kubadilisha sura ya soka ya Afrika kwa kujadili hali na viwango vya mchezo huo, kutathmini mbinu za kibiashara na kutoa mwelekeo dhabiti wa uongozi katika mashirikisho ya mpira, teknolojia mchezoni na ukuzaji talanta.

Kongamano hilo lilihudhuriwa na washikadau kutoka mataifa mbali mbali duniani ikiwemo Ufaransa, Rwanda, Kenya, Ghana, Zimbabwe, Afrika Kusini, Ujerumani, Chille, Misri, Chad na wawakilishi kutoka shirikisho la soka duniani FIFA.

Uwajibikaji na ukuzaji talanta

Anthony Baffoe, beki wa zamani wa timu ya taifa ya Ghana ambaye amewahi kuhudumu kama naibu katibu mkuu katika shirikisho la soka barani Afrika CAF, amesisitiza umuhimu wa uwajibikaji kwa viongozi wote wa soka.

Usipowajibika, FIFA na CAF watafanya uchunguzi wao na utajipata matatani, litakalofuata ni kupigwa marufuku ambayo itaua talanta za soka barani

Baffoe aidha aliorodhesha umuhimu wa kuwa na umoja, kuelimishana na kusambaza ujumbe na maarifa kwa vizazi vijavyo. Katika sekta ya ukuzaji talanta, kadhalika alisisitiza umuhimu wa kujifunza kutoka kwa mabara mengine yanazofanya vizuri pamoja na  pia  kutafuta mianya zaidi kwenye ukuzaji talanta kwa mfano kuanzisha chuo cha mafunzo ya michezo na kuziandikisha katika mashirikisho ya ndani, mfano  jinsi CAF na FIFA zimependekeza, kila klabu ni sharti ifuate kanuni za kuwa na leseni ya CAF (CAF Club Licensing)

Udhamini na Uwekezaji

Kwa mfano soka la Kenya linayumba kwa sababu mojawapo ikiwa ni ukosefu wa wadhamini na wawekezaji wa kutosha, kongamano hilo pia lilipendekeza njia tofauti za kuvutia wadhamini.

Kupakwashe Mukurumbira mwakilishi wa Dominion Sports, nchini Zimbabwe, alitoa ramani ya kuchukulia soka kitaaluma kama taaluma zingine duniani.

Wafanyabiashara wa soka ni muhimu sana kwani wao ndio wanatengeneza mazingira ya kuvutia wadhamini na wawekezaji, ni muhimu tuwalete karibu na tuwahusishe pakubwa,

alisema Mukurumbira.

Kupakwashe alipendekeza ushirikiano dhabiti na wadhamini wa ndani pamoja pia na wale wa kimataifa kathalika na akisema hilo litarembesha soka ya Afrika na  wanahabari kuandika kuhusu matukio ya michezo barani mara kwa mara., na kushauri kwamba vilabu  vinafaa viwe na sekta yao binafsi ya uanahabari ili kuongeza nguvu kwenye utoaji wa taarifa sababu itavutia mashabiki pakubwa.

Usimamizi wa kimantiki na Uboreshwaji wa ligi za Afrika

Patrick Korir, mkurugenzi mkuu wa klabu ya Nairobi City Stars nchini Kenya alieleza umuhimu wa kupanga mikakati kabambe ya wakati huu na miaka ijayo pamoja pia na kutojiwekea malengo ambayo vigumu kuyaafikia. Kwa mfano kwenye klabu yake alipoteuliwa kuwa mkurugenzi mtendaji alimwambia bwenyeye wa klabu kuwa si rahisi kukamilisha uhamisho wa wachezaji kumi au zaidi nje ya Kenya kwa miaka mitatu bali huenda ikawa hata vigumu kwa mchezaji mmoja.

Ni malengo kama hayo ya kiuhalisia yaliyoiwezesha City Stars kukamilisha uhamisho wa kiungo wa kati Sven Yidah Sven kuelekea Marumo Gallants ya Afrika Kusini pamoja na wachezaji wengine wachache.

Jeremy Cottino ambaye ni afisa mkuu wa uendeshaji katika klabu ya AS Monaco ya Ufaransa alielezea njia tofauti za kuboresha usimamizi wa wachezaji kwenye vilabu.

Kitu cha kwanza ni kubaini klabu ni ya aina gani, thamani, mashabiki wao ni kina nani kisha malengo yako ni gani tuseme kwa miaka mitano au kumi ijayo, huo ndio mwanzo wa safari hii ya usimamizi wa klabu

 Rogers Munyampenda mshauri wa michezo na mtaalamu wa mikakati ya biashara kutoka Rwanda alimuunga mkono Jeremy kwa kusisitiza kuwa ili ligi zetu ziwe bora, kitu cha kwanza ni kuendeleza mjadala kati ya umma na mashirikisho na tujenge mfumo wa maendelezo, tuwalete washikadau wote pamoja tuweke mlengo yetu na tujikite kuyaafikia kisha tujiwekee viwango vya uwajibikaji ili tujue tutakapokuwa kwa miaka mitano au kumi ijayo.

Soko la Uhamisho wa wachezaji

Hector Navarro mwakilishi wa FIFA alisema kufikia mwaka 2010, uhamisho wa wachezaji 10,000 ulifanyika na hadi sasa idadi hiyo imeongezeka karibu maradufu hadi 18,000.

Bara la Ulaya linaongoza kwenye uhamisho wa wachezaji likifuatiwa na bara la Marekani Kusini, Kulingana na Hector, bara Afrika  limefanya uhamisho wa ndani takriban 25,000 kati ya mataifa ya Afrika pekee, aliliorodhesha kwa  nafasi ya tatu baada ya Ulaya na Marekani Kusini.

Misri ni miongoni mwa mataifa thelathini yanayopokea kiasi kikubwa cha ada za uhamisho, Nigeria na Ghana ni miongoni mwa mataifa 25, Lakini je, Afrika inastahili kufanya nini ili kunufaika kwenye soko la uhamisho wa wachezaji?

Kitu cha kwanza, Afrika inafaa kuwekeza pakubwa kwenye mazoezi ya wachezaji na mshikamano wao kabla ya kujikita sana kwenye ada za uhamisho. Pili, Afrika inahitaji kuwe na mfumo maalum wa kidijitali wa uhamisho wa wachezaji ili iwe rahisi kufuatilia safari ya mchezaji kwenye taaluma hii ya soka

Hector Navarro alisisitiza.

Teknolojia kwenye soka

Maudhui ya teknolojia kwenye soka yalijadiliwa kwa nia ya kutumia teknolojia vizuri kwani dunia inabadilika kila kuchao.

Mitandao ya kijamii kwa vilabu au vyuo ni njia mwafaka sana ya kujiuza na kujitangaza kwenye ulimwengu wa soka.

Mashirikisho yakifanikiwa kupeperusha mechi zao kwenye runinga itasaidia pakubwa katika ukuaji wa soka la Afrika.

Tazama wafuasi wa vilabu kama Manchester United, PSG, Barcelona, Bayern Munich kisha ulinganishe na vilabu vya Afrika kama TP Mazembe, Gor Mahia, Simba SC, Yanga SC, Vipers SC, Rayon Sports, AFC Leopards, na kadhalika utagundua kuna utofauti mkubwa sana.

Qatar 2022

Bila kusahau, zinasalia siku 27 kuanza kwa mashindano ya kombe la dunia nchini Qatar ambapo Afrika itawakilishwa na mataifa matano – Cameroon, Senegal, Ghana, Tunisia na Morocco, Anthony Baffoe alitoa ujumbe spesheli kwa mashabiki wa soka barani Afrika.

Nakumbuka mwaka 1990 nilikuwa Ujerumani na Afrika iliwakilishwa na Cameroon pekee na walifanya vizuri sana sababu bara zima lilikuwa linawashabikia, Nafikiri jukumu kubwa la mashabiki wote ni kushabikia timu zote tano bila kuchagua sababu sisi sote ni waafrika, Hilo litatoa motisha sana kwa bara Afrika kwa ujumla kufika mbali mashindanoni

Kongamano hilo lilikamilika siku ya pili kwa warsha wa kutambua talanta na ukuzaji wa talent hizo kwa makocha, mawakala na viongozi wa akademia za soka.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.