Pata taarifa kuu
KENYA-IAAF-RIADHA-DUNIA

Kenya kuwa mwenyeji wa mashindano ya riadha ya dunia kwa vijana chini ya miaka 20

Shirikisho la riadha duniani IAAF limeichagua Kenya kuwa mwenyeji wa mashindano ya riadha ya dunia kwa vijana wasiozidi miaka 20, itakayofanyika mwaka 2020.

Uwanja wa Kimataifa wa Kasarani jijini Nairobi
Uwanja wa Kimataifa wa Kasarani jijini Nairobi www.iaaf.org
Matangazo ya kibiashara

Rais wa IAAF Sabastian Coe, ametangaza hatua hiyo baada ya mkutano Mkuu wa Baraza la mchezo huo uliofanyika siku ya Ijumaa jijini Buenos Aires nchini Argentina.

Jiji la Nairobi limepata fursa nyingine ya kuandaa mashindano makubwa duniani baada ya mwaka 2017 kufanikisha wenyeji wa mashindano ya dunia kwa vijana wasiozidi miaka 18.

Mashindano hayo yatafanyika katika uwanja wa Kimataifa wa Michezo wa Kasarani jijini Nairobi.

Mashabiki 60,000 wanatarajiwa kushuhudia mashindano hayo kama ilivyokuwa mwaka 2017.

Katibu katika Wizara ya Michezo nchini humo Kirimi Kaberia amesema Kenya ni nyumbani kwa mchezo wa riadha na muhimu kwa maisha ya wananchi wa taifa hilo.

“Riadha ni mchezo muhimu sana kwa maisha yetu. Kila mtu anapenda riadha nchini Kenya.Mliona wakati wa mashindano ya wanariadha chini ya miaka 18 na mtaona tena mwaka 2020,” amesema Kaberia.

Rais Uhuru Kenyatta amefurahia uamuzi wa IAAF na kupitia ukurasa wake wa Twitter ameikaribisha dunia nchini Kenya mwaka 2020.

Mashindano hayo yamepangwa kufanyika kati ya Julai tarehe 7-12.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.