Pata taarifa kuu
CAF-SOKA

TP Mazembe na MO Bejaia zafuzu hatua ya nusu fainali taji la Shirikisho

Timu za soka za Etoile du Sahel ya Tunisia, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, MO Bejaia ya Algeria na FUS Rabat ya Morroco, zimefuzu katika hatua ya nusu fainali kuwania taji la Shirikisho barani Afrika.

Wachezaji wa klabu ya TP Mazenbe wakisherehekea baada ya kufuzu katika hatua ya nusu fainali taji la Shirikisho barani Afrika Agosti 24 2016
Wachezaji wa klabu ya TP Mazenbe wakisherehekea baada ya kufuzu katika hatua ya nusu fainali taji la Shirikisho barani Afrika Agosti 24 2016 static.goal.com
Matangazo ya kibiashara

Hatua hii inakuja baada  ya kumalizika kwa mechi za hatua ya makundi siku ya Jumanne.

Mazembe wakicheza nyumbani mjini Lubumbashi, waliwafunga Yanga FC ya Tanzania mabao 3-1 na kumaliza kundi la A kwa alama 13.

Mabao ya Mazembe yalitiwa kimyani na Jonathan Bolingi katika dakika ya 28 ya mchuano huo, huku Rainford Kalaba akiipa timu yake mabao mawili katika kipindi cha pili mnamo dakika ya 55 na 63.

Bao la pekee la kufutia machozi  la Yanga FC, lilifungwa na Hamis Tambwe katika dakika ya 75 ya mchuano huo.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa Yanga FC kufika katika hatua hii ya makundi katika michuano hii; katika historia yake ya soka na kumaliza ya mwisho katika kundi lao kwa alama 4, baada ya kushinda mechi moja, kwenda sare mchuano mmoja na kushindwa michuano minne.

Ilikuwa bahati mbaya kwa Medeama FC ya Ghana baada ya kupoteza ugenini bao 1-0 dhidi ya MO Bejaia iliyofuzu kwa alama nane, kwa wingi wa mabao.

Nembo ya shirikisho barani Afrika CAF
Nembo ya shirikisho barani Afrika CAF kwesesport

FUS Rabat na Etoile du Sahel nazo zilitoka sare ya kutofungana katika mchuano wao.

Etoile du Sahel itamenyana na TP Mazembe katika hatua ya nusu fainali nyumbani na ugenini, huku MO Bejaia ikipambana na FUS Rabat mwezi Septemba.

Katika michuano ya klabu bingwa, Zamalek ya Misri na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini zinasubiri wapinzani wao katika hatua hii ya nusu fainali baada ya mechi ya Jumatano.

ASEC Mimosas ya Ivory Coast inacheza na Al Ahly ya Misri, zote ambazo zimeshaondolewa huku ZESCO ya Zambia ikichuana na Wydad Casablanca ya Morroco.

Zamelek itacheza na mshindi wa kundi A , ZESCO au Wydad Casablanca huku Mamelodi Sundowns ikimsubiri mshindi wa pili katika kundi hilo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.