Pata taarifa kuu
RIO OLIMPIKI 2016

RIO OLIMPIKI; Phelps afanya kweli, Serena atupwa nje, Marekani yatwaa medali mchezo wa Sarakasi

Muogeleaji Michael Phelps raia wa Marekani, ameendelea kuweka rekodi kwenye mchezo huo baada ya usiku wa kuamkia Jumatano ya Agosti 10, kujinyakulia medali yake ya 20 na 21 ya dhahabu akiwa peke yake na nyingine akiwa na timu ya Marekani, katika siku ya 4 ya michezo ya Olimpiki ya Rio, Brazil. 

Muogeleaji wa Marekani, Michael Phelps aking'ata medali yake ya dhahabu baada ya kushinda kuogelea mtindo wa freestyle, 9 Agosti, 2016
Muogeleaji wa Marekani, Michael Phelps aking'ata medali yake ya dhahabu baada ya kushinda kuogelea mtindo wa freestyle, 9 Agosti, 2016 REUTERS/Marcos Brindicci
Matangazo ya kibiashara

Phelps mwenye umri wa miaka 31, alimshinda bingwa mtetezi Chad le Clos katika mita 200 mtindo wa butterfly, kabla ya kuisaidia timu yake ya Marekani kushinda medali ya dhahabu kwenye mita 4x200 mtindo wa freestyle kwa upande wa wanaume.

Waingereza Stephen Milne, Duncan Scott, Dan Wallace na James Guy walishinda medali ya fedha katika mtindo wa Relay.

Akizungumza mara baada ya kushinda medali hizo, Phelps alesema "sikiliza! Phelps amerudi kwenye ufalme wake."

Timu ya kuogelea ya Marekani ambayo imeshinda medali ya dhahabu, 9 Agosti, 2016
Timu ya kuogelea ya Marekani ambayo imeshinda medali ya dhahabu, 9 Agosti, 2016 REUTERS/Michael Dalder

Phelps alianza usiku wake kwa kumshinda mpinzani wake wa karibu Le Clos aliyemuangusha wakati wa michezo ya Olimpiki ya London mwaka 2012.

"Nilitaka kwanza kurejesha taji langu. Nilikuja kwenye bwawa la kuogelea leo hii nikiwa na misheni, misheni moja tu ambayo niliikamilisha vizuri." alisema muogeleaji huyo.

Mjapan Masato Sakai na Muhungary Tamas Kenderesi walimpiku Le Clos katika mita 50 za mwisho kushinda medali ya fedha na shaba.

Phelps na Le Clos watakutana tena baadae wiki hii katika kuwania medali kwenye mita 100 mtindo wa butterfly, ambapo pia, Phelps atakuwa akijaribu kuchukua medali nyingine ya dhahabu wakati atakaposhiriki mita 4x100 na 200 mtindo wa medley akiwa na timu na medley akiwa binafsi.

Katika tenesi bingwa mtetezi Serena Williams alitupwa nje ya michezo ya Olimpiki ya Rio baada ya kupoteza mchezo wake mbele ya Elina Svitolina kutoka Ukraine kwenye mzunguko wa tatu upande wa wanawake.

Serena Williams akiwa anatoka uwanjani ameinamisha kichwa baada ya kupoteza mchezo wake kwenye michezo ya Rio, 9 Agosti, 2016
Serena Williams akiwa anatoka uwanjani ameinamisha kichwa baada ya kupoteza mchezo wake kwenye michezo ya Rio, 9 Agosti, 2016 REUTERS/Kevin Lamarque

Williams alipoteza mchezo huo kwa matokeo ya seti mbili kwa bila kwa matokeo ya 6-4 na 6-3, Svitolina anashikilia nafasi ya 20 kwa ubora wa mchezo huo duniani kwa upande wa wanawake.

Kutolewa kwa Serena kunakuja ikiwa ni siku mbili tu zimepita toka yeye na dada yake watolewe kwenye michezo hiyo.

Katika mchezo wa sarakasi, timu ya Marekani kwa mara nyingine iliishangaza dunia baada ya kufanikiwa kutetea taji lake, baada ya kupata alama 184.897, likiwa ni taji lao la 5 la kidunia.

Mmarekani, Simone Biles  akionesha umahiri wake wakati wa michezo ya rio, mchezo wa Sarakasi, aliisaidia nchi yake kutwaa medali ya dhahabu, 9 Agosti, 2016
Mmarekani, Simone Biles akionesha umahiri wake wakati wa michezo ya rio, mchezo wa Sarakasi, aliisaidia nchi yake kutwaa medali ya dhahabu, 9 Agosti, 2016 REUTERS/Dylan Martinez

Timu ya Urusi yenyewe ilijinyakulia medali ya fedha kwa kupata alama 176.688 mbele ya timu ya China iliyojinyakulia medali ya shaba kwa kupata alama 176.003 na Japan ikipata alama 174.371, huku timu ya Uingereza iliyokuwa inasaka medali yake ya kwanza toka mwaka 1928 ilimaliza kwenye nafasi ya nne kwa kupata alama 174.362.

Mpaka sasa Marekani inaongoza kwa kuwa na medali 26 kwa ujumla, ikifuatiwa na Uchina yenye medali 17, Hungary yenye medali 16, Australia yenye medali 9, Urusi yenye medali 12, Italia yenye medali 9, Korea Kusini ina medali 16, Japan ina medali 14, Ufaransa ina medali 6 na Thailand yenye medali 4.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.