Pata taarifa kuu
SOKA

Orlando Pirates na Al Ahly kumenyana Jumamosi usiku kutafuta ubingwa wa CAF

Klabu ya soka ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini Jumamosi hii itakuwa wenyeji wa mabingwa watetezi wa taji la klabu bingwa barani Afrika Al Ahly ya Misri katika fainali ya mchuano wa mzunguko wa kwanza kuwania taji hilo. 

Matangazo ya kibiashara

Mchuano huo utachezwa katika uwanja wa Orlando katika mtaa wa Soweto jijini Johannesburg kuanzia saa mbili na nusu usiku saa za Afrika ya Kati.

Timu hizi mbili zinakutana katika mchuano wa fainali baada ya kukutana mara mbili katika michuano ya makundi msimu huu.

Katika mchuano wa kwanza, Orlando Pirates wakiwa ugenini waliwafunga Al Ahly mabao 3 kwa 0 mjini El Gouna mwezi Agosti na baadaye wakatoka sare ya kutofungana katika mchuano wa marudiano uliochezwa mwezi Septemba katika uwanja wao wa nyumbani wa Orlando Stadium.

Pirates waliwashinda mabingwa wa soka nchini Tunisia Esperance kwa sheria ya bao la ugenini baada ya kutoka sare ya bao 1 kwa 1 katika mchuano wa mzunguko wa mwisho.

Al Ahly nayo ilifuzu baada ya kuishinda Coton Sport ya Cameroon kwa mikwaju penalti kwa kuwafunga mabao 7 kwa 6 baada ya kutoka sare ya mabao 2 kwa 2 katika muda wa kawaida.

Kocha wa Pirates Roger de Sa amesema kuwa hatua ya klabu yake kufika fainali kunaonesha uwezon wa wachezaji wake na wana uwezo wa kupata ushindi wa kuridhisha Jumamosi usiku mbele ya Al Alhy ambayo imefika fainali ya CAF mara tisa.

Mzunguko wa mwisho wa mchuano huo utachezwa tarehe 10 mwezi Novemba ambapo Al Ahly watakuwa wenyeji wa Orlando Pirates katika uwanja wao wa nyumbani mjini El Gouna.

Mshindi ataliwakilisha bara la Afrika katika michuano ya dunia ya klabu bingwa ,itakayofanyika kati ya tarehe 11 hadi 21 mwezi ujao nchini Morroco.

Vlabu ambavyo tayari vimefuzu katika michuano hiyo ni pamoja na Bayern Munich, Atletico Mineiro, Monterrey, Auckland City na wenyeji Raja Casablanca.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.