Pata taarifa kuu

Jeshi la Israel lawaonya wakazi wa kaskazini mwa Ukanda wa Gaza

Jeshi la Israel linawaonya wakaazi wa Gaza ambao hawajaondoka kaskazini mwa Ukanda wa Gaza. Katika video kwenye X mapema mchana, mmpja wa wasemaji wa jeshi la Israel, Daniel Hagari, amerejelea wito wa Israel kwa wakaazi wa Kaskazini kwa Ukanda wa Gaza na Jiji la Gaza kuelekea kusini mwa eneo hilo.

Jeshi la Israel likirusha makombora kuelekea Ukanda wa Gaza mnamo Oktoba 28, 2023.
Jeshi la Israel likirusha makombora kuelekea Ukanda wa Gaza mnamo Oktoba 28, 2023. AFP - ARIS MESSINIS
Matangazo ya kibiashara

“Tahadharini, wananchi wa Gaza, sikilizeni kwa makini. Hili ni onyo la dharura la kijeshi kutoka kwa Jeshi la Ulinzi la Israeli. Kwa usalama wanu wa haraka, tunawaomba wakaazi wote wa kaskazini mwa Ukanda wa Gaza na Jiji la Gaza kuhamia kusini kwa muda. Kurudi kaskazini mwa Gaza kutawezekana mara tu mapigano makali [yatakapomalizika]. "

Wakati huo huo Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant amesema leo Jumamosi kwamba vita dhidi ya kundi la Hamas kutoka Palestina "vimeingia katika awamu mpya" baada ya usiku wa mashambulizi makali ya anga na uvamizi wa jeshi la Israel katika Ukanda wa Gaza. “Tumeingia katika awamu mpya katika vita. Jana, ardhi katika Ukanda wa Gaza ilitikisika,” Yoav Gallant amesema katika video iliyochapishwa na idara zake.

Tangu Ijumaa jioni, Oktoba 27, jeshi la Israel limekuwa likifanya mashambulizi makali ya anga kwenye Ukanda wa Gaza. Mnamo Oktoba 28, mawasiliano katika eneo lililozingirwa bado yamekatwa.

Viongozi kadhaa walaani operesheni za Israel

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ametangaza wakati wa "mkutano wa kuunga mkono Palestina", ambao uliwaleta pamoja watu laki kadhaa katika uwanja wa ndege wa zamani wa Atatürk huko Istanbul, kwamba Israeli inakalia kwa mabavu maeneo ya Palestina na kusisitiza msimamo wake kwamba Hamas sio kundi la kigaidi. "Ninasisitiza kwamba Hamas sio kundi la kigaidi. Israeli walichukizwa sana na jambo hili. [...] Israel ni inakalia kwa mabavu maeneo ya Palestina, Erdogan anazungumza waziwazi kwa sababu Uturuki haina deni lolote kwako,” amesema mbele ya mamia ya maelfu ya wafuasi wake. Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan pia ameshutumu nchi za Magharibi kuwa "wahusika wakuu wa mauaji huko Gaza." "Ukiondoa watu wachache waliopaza sauti zao, mauaji haya ni kazi ya nchi za Magharibi," amesema rais wa Uturuki.

Waandamanaji wakati wa maandamano ya mshikamano na Wapalestina, huku kukiwa na mzozo unaoendelea kati ya Israel na kundi la Kiislamu la Hamas kutoka Palestina, mjini Istanbul, Uturuki, Oktoba 28, 2023.
Waandamanaji wakati wa maandamano ya mshikamano na Wapalestina, huku kukiwa na mzozo unaoendelea kati ya Israel na kundi la Kiislamu la Hamas kutoka Palestina, mjini Istanbul, Uturuki, Oktoba 28, 2023. © Dilara Senkaya / Reuters

Kwa upande wake Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudia imetoa taarifa siku ya Jumamosi ikilaani operesheni zozote za ardhini zinazofanywa na wanajeshi wa Israel ambazo zinaweza kutishia maisha ya raia wa Palestina. "Saudia inalaani na kushutumu operesheni za ardhini zinazofanywa na jeshi la Israel katika Ukanda wa Gaza, na kuonya juu ya hatari ya kuendelea kutekeleza ukiukwaji huu wa wazi na usio na msingi wa sheria za kimataifa dhidi ya ndugu zetu wa Palestina," ilmesema taarifa hiyo.

Umoja wa Mataifa unahofia "maelfu ya vifo vingine vya raia" huko Gaza katika tukio la operesheni kubwa ya ardhini. "Kwa kuzingatia jinsi operesheni za kijeshi zimetekelezwa hadi sasa, katika muktadha wa uvamizi wa miaka 56, nina hofu juu ya matokeo ya uwezekano wa janga la operesheni kubwa za ardhini huko Gaza na kuna uwezekano operesheni hiyo itasababisha maelfu zaidi ya vifo vya raia,” ameandika Volker Türk katika taarifa iliyotolewa Geneva.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza yanakwenda kinyume na sheria za kimataifa na hatari ya kusababisha janga ambalo linaweza kudumu kwa miongo kadhaa. Ameyasema hayo katika mahojiano na shirika la habari la serikali la Belarusian Belta, ambalo lilichapisha Jumamosi, na kutangazwa na shirika la habari la REUTERS.

"Wakati tunalaani ugaidi, hatukubaliani kabisa kwamba ugaidi unaweza kushughulikiwa kwa kukiuka kanuni za sheria za kimataifa za kibinadamu, ikiwa ni pamoja na kutumia nguvu kwa njia ya kiholela dhidi ya walengwa ambapo inajulikana kuwa raia wapo, ikiwa ni pamoja na mateka ambao wamechukuliwa" , Lavrov amesema.

"Haiwezekani," ameongeza, "kuangamiza Hamas - kama Israel imejitolea kufanya - bila kuharibu Gaza na idadi kubwa ya raia wake. Iwapo Gaza itaharibiwa na wakaazi milioni mbili kufukuzwa, kama wanavyopendekeza baadhi ya wanasiasa nchini Israel na nje ya nchi, hili litazua maafa ambayo yatadumu kwa miongo kadhaa, hata karne nyingi,” Lavrov ameonya kwamba Urusi pia ilikuwa na mawasiliano ya karibu na Israel. “Tunasalia katika mawasiliano kamili na Israel, na balozi wetu anawasiliana nao mara kwa mara. Tunatuma ujumbe juu ya hitaji la kutafuta suluhisho la amani na sio kufuata mkakati uliotangazwa wa ardhi iliyoteketea kwa moto. "

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.