Pata taarifa kuu

Kuanzia Cairo hadi Baghdad, ulimwengu wa Kiarabu waandamana kuunga mkono Gaza

Kuanzia Cairo hadi Baghdad kupitia Tunis, makumi ya maelfu ya watu wameandamana siku ya Ijumaa katika miji mikuu ya nchi za Kiarabu kuunga mkono Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, unaoshambuliwa na Israel tangu shambulio la Hamas.

Maandamno mjini Cairo ili kuonyesha mshikamano na watu wa Gaza baada ya sala ya Ijumaa kwenye Msikiti wa Azhar, taasisi ya kwanza ya Kiislamu katika ulimwengu wa Kiislamu wa Sunni, Oktoba 20, 2023.
Maandamno mjini Cairo ili kuonyesha mshikamano na watu wa Gaza baada ya sala ya Ijumaa kwenye Msikiti wa Azhar, taasisi ya kwanza ya Kiislamu katika ulimwengu wa Kiislamu wa Sunni, Oktoba 20, 2023. AP - Amr Nabil
Matangazo ya kibiashara

Zaidi ya watu 1,400 wameuawa nchini Israeli na wanamgambo wa Kiislamu wa Hamas tangu Oktoba 7, raia wengi waliuawa kwa risasi, kuchomwa moto wakiwa hai au kuuawa kwa kukatwa viungo vyao katika siku ya kwanza ya shambulio la kundi hili la wanamgambo wa Kiislamu la Hamas kutoka Palestina lililotekelezwa kutoka Gaza, kulingana na mamlaka ya Israeli.

Kwa mujibu wa jeshi la Israel, karibu wapiganaji 1,500 wa Hamas waliuawa katika mashambulizi hayo ambayo yaliiwezesha Israel kutwaa tena udhibiti wa maeneo yaliyoshambuliwa. Katika Ukanda wa Gaza, zaidi ya Wapalestina 4,100, wengi wao wakiwa nia raia, wameuawa katika mashambulizi ya mara kwa mara ya kulipiza kisasi na jeshi la Israel, kwa mujibu wa mamlaka ya ndani.

Siku ya Ijumaa, Umoja wa Mataifa umekuwa ukitayarisha kupitishwa kwa misaada ya kimataifa inayosubiriwa kwa hamu na wakaazi milioni 2.4 wa Gaza, eneo dogo lililonyimwa kila kitu. Baada ya sala ya Ijumaa, makumi ya maelfu ya watu waliingia barabarani "kuunga mkono Gaza" katika miji ya nchi za Kiarabu, siku mbili baada ya "siku ya hasira" ambayo tayari ilikuwa na maandamano mengi.

Huko Cairo, makumi ya maelfu ya waandamanaji, ikiwa ni pamoja na elfu chache katika eneo la Tahrir Square, waliimba "Mkate, uhuru, Palestina ya Kiarabu" na "Watu wanataka kufutwa kwa taifa la Israeli".

Maandamano nchini Iraq

Katika siku ya 14 ya vita kati ya Israel na Hamas mamlakani huko Gaza, maandamano pia yalifanyika katika miji mingi nchini Misri, kulingana na vyombo vya habari vya ndani. Huko Baghdad, maelfu ya watu waliandamana, wakiwemo wafuasi wengi wa Hachd al-Chaabi, muungano wa makundi yenye silaha yenye uhusiano wa karibu na Iran, adui mkuu wa Israel na mfuasi wa Hamas.

Waandamanaji hao walikusanyika mbele ya daraja linaloelekea eneo la Green Zone, sekta iliyoimarishwa ambayo ina makao ya ubalozi wa Marekani, nchi inayochukiwa na makundi yanayoiunga mkono Iran kwa uungaji wake mkono kwa Israel. "Tunaunga mkono watu wa Palestina dhidi ya eneo la Israel linaloikalia kwa mabavu," Ali Hussein, dereva wa teksi mwenye umri wa miaka 45, ameliambia sjirika la habari la AFP.

Maandamano pia yalifanyika katika majimbo ya Iraq ya Ninawi (kaskazini) na Dhi Qar (kusini). Magharibi mwa nchi, karibu na mpaka na Jordan, wafuasi mia chache wa Hachd al-Chaabi walianza kuketi mbele ya ofisi za serikali ishara ya "kuunga mkono Gaza".

"Ufaransa, ondoka."

Hasira pia ilitanda nchini Jordan, nchi jirani ya Israel ambayo inahusishwa na mkataba wa amani. Katika mji mkuu wa Amman, zaidi ya watu 5,000 walikusanyika mbele ya Msikiti Mkuu wa Husseini wakiimba "Okoeni Gaza!" na "Fungueni mipaka kusaidia watu wa Palestina."

Huko Tunis, maelfu ya waandamanaji walikusanyika mbele ya ubalozi wa Ufaransa, nchi inayoshutumiwa kuiunga mkono Israel katika vita vyake dhidi ya Hamas. "Ufaransa, ondoka", "Watu wanataka kufutwa kwa balozi (ya Ufaransa)", waliimba, huku wakionyesha uungaji wao mkono kwa Hamas.

Makumi ya waandamanaji wengine walikusanyika karibu na ubalozi wa Marekani katika viunga vya kaskazini mwa Tunis na kuchoma bendera ya Marekani. Polisi waliwazuia kukaribia ubalozi, kulingana na vyombo vya habari vya ndani. Katika Bahrain, nchi ndogo ya Ghuba, karibu watu 2,000 walipaza sauti "Israeli wafu!" na "Marekani wafu" katika Msikiti wa Diraz.

"Mimi ni mama, siwezi kufikiria ukatili ambao familia huko Gaza zinapitia," amesema mmpja wa waandamanaji, akiwa na mtoto mchanga mikononi mwake, wakati wa maandamano yaliyoandaliwa baada ya sala. "Tunataka mwisho wa uhusiano na Israel na kufukuzwa kwa balozi wa Israeli," ameongeza, akimaanisha Mkataba wa Abraham wa 2020, uliojadiliwa na Marekani, ambao ulipelekea Bahrain, Falme za Kiarabu, kisha Morocco, kuanzisha uhusiano rasmi pamoja na Israeli.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.