Pata taarifa kuu

Syria: Zaidi ya watu 110 wauawa katika shambulio dhidi ya jeshi,

Zaidi ya watu 110 waliuawa siku ya Alhamisi Oktoba 5, 2023 katika shambulio dhidi ya chuo cha kijeshi nchini Syria, wakati ambapo Uturuki ilifanya mashambulizi dhidi ya maeneo ya Wakurdi ambayo yalisababisha vifo vya takriban watu 11.

Mtu aliyejeruhiwa wakati wa shambulio la ndege isiyo na rubani kwenye sherehe katika chuo cha kijeshi cha Homs kilio chini ya udhibiti wa utawala wa Syria, Oktoba 5, 2023.
Mtu aliyejeruhiwa wakati wa shambulio la ndege isiyo na rubani kwenye sherehe katika chuo cha kijeshi cha Homs kilio chini ya udhibiti wa utawala wa Syria, Oktoba 5, 2023. © AFP PHOTO / HO / SANA
Matangazo ya kibiashara

Jeshi la Syria limehusisha shambulio hilo dhidi ya sherehe za kupandishwa vyeo kwa maafisa wa serikali huko Homs kwa"makundi ya kigaidi". Jeshi limeahidi "kujibu shambulizi hilo haraka iwezekanavyo". Shambulio hilo lilitekelezwa "kwa kutumia ndege zisizo na rubani zilizojaa vilipuzi", kulingana na jeshi.

Shambulio hilo lilisababisha vifo vya watu 112, wakiwemo raia 21 na takriban 120 kujeruhiwa, kwa mujibu wa ripoti mpya ya shirika la Haki za Binadamu la Syrian Observatory for Human Rights (OSDH), shirika lenye makao yake nchini Uingereza lenye mtandao mkubwa kutoka vyanzo nchini Syria. Waziri wa Afya wa Syria Hassan al-Ghobash alitangaza idadi "ya awali" ya watu 80 walioangamia katika shambulio hilo, "ikiwa ni pamoja na wanawake sita na watoto sita", na karibu 240 kujeruhiwa. Shambulio hilo halijadaiwa na kundi lolote. Makundi ya kijihadi yanayodhibiti sehemu ya ardhi ya Syria wakati mwingine hutumia ndege zisizo na rubani.

Vikosi vya serikali vimejibu kwa mashambulizi ambayo, kulingana na wakazi, yalilenga eneo la Idleb, ngome ya mwisho ya waasi nchini humo, kaskazini magharibi. OSDH imeripoti vifo vinane na 30 kujeruhiwa.

Wakati huo Uturuki yashambulia maeneo ya wakurdi kaskazini mwa Syria 

Siku ya Alhamisi, ndege zisizo na rubani za Uturuki zililenga maeneo ya mafuta, vinu viwili vya kuzalisha umeme, bwawa na kiwanda kimoja katika mkoa wa Hassake, unaodhibitiwa na wapiganaji wa SDF, muungano unaotawaliwa na Wakurdi. Vikosi vya Wakurdi vimetangaza kuwa Uturuki vimefanya mashambulizi 21 na kusababisha vifo vya watu 11 wakiwemo raia watano na maafisa sita wa vikosi vya usalama.

Jioni, vyombo vya habari vya Uturuki viliripoti mashambulizi mapya ya Uturuki dhidi ya vikosi vya Wakurdi nchini Syria, vikidai kwamba "ghala za silaha na risasi za PKK/YPG ziliharibiwa" wakati wa operesheni iliyoongozwa na vitengo vya MIT, idara za kijasusi. Uturuki inadai kulipiza kisasi shambulizi lililolenga Wizara ya Mambo ya Ndani huko Ankara siku ya Jumapili, na kuwajeruhi maafisa wawili wa polisi. Kulingana Uturuki, wahusika wa shambulio hilo, linalodaiwa na Chama cha Wafanyakazi wa Kurdistan (PKK, Wakurdi wa Kituruki), walipata mafunzo nchini Syria, shutuma zilizokanushwa na kiongozi wa FDS, Mazloum Abdi.

Mzozo wa Syria ulioanza mwaka 2011 umesababisha vifo vya watu zaidi ya nusu milioni na kuigawanya nchi hiyo ambapo Marekani, Urusi, mshirika wa utawala huo, na Uturuki zimepeleka wanajeshi katika maeneo tofauti.

(Pamoja na AFP)

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.