Pata taarifa kuu

Nyuklia: Mpango wa Iran wakaribia kizingiti cha silaha ya atomiki kulingana na IAEA

Katika ripoti yake ya hivi punde iliyochapishwa Jumanne, Februari 28, Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) linasema kuwa Iran inaendelea na mpango wake wa kurutubisha uranium kwa kasi kubwa. Shirika hili limegundua chembe za uranium iliyorutubishwa kwa 83.7%, kizingiti karibu na kiwango cha 90% kinachotumiwa kutengeneza silaha za atomiki. Tehran imekanusha.

Mohammad Eslami, mkurugenzi wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran, akizungumza katika mkutano wa shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki huko Vienna, Austria, Septemba 26, 2022.
Mohammad Eslami, mkurugenzi wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran, akizungumza katika mkutano wa shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki huko Vienna, Austria, Septemba 26, 2022. AP - Theresa Wey
Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa ripoti ya IAEA, akiba ya madini ya uranium iliyorutubishwa nchini Iran sasa imevuka kikomo kilichoidhinishwa na makubaliano ya nyuklia ya 2015 kwa mara 18. Tehran hasa ina kilo 87 za uranium iliyorutubishwa hadi 60%. Zaidi ya yote, shirika la Umoja wa Mataifa limegundua chembe za uranium iliyorutubishwa kwa kiwango cha karibu na 90%, kizingiti muhimu cha kuzalisha bomu la atomiki.

Takwimu hizi mpya zinatishia nchi za Magharibi. Kulingana na mkuu wa CIA, shirika la ujasusi la Marekani, Iran inaweza, katika wiki chache, kutoa uranium iliyorutubishwa ya kutosha kutengeneza bomu la atomiki.

Iran imekanusha tuhuma hizi. Msemaji wa mpango wa nyuklia Behrouz Kamalvandi amesema ni chembe ndogo mbili au tatu tu zenye urutubishaji zaidi ya 84% ndizo ziligunduliwa kwenye eneo la Fordoo, jambo ambalo ni la kawaida. "Ikiwa tungetaka kurutubisha zaidi ya 60% tungesema hadharani," ameongeza.

Ripoti ya IAEA imechapishwa wakati mkuu wake, Rafael Grossi, anatarajiwa kuzuru Tehran katika siku zijazo. Iran imeweka wazi kuwa hakuna suala la kuweka kikomo mpango wake wa nyuklia hadi Marekani ikubali kuondoa vikwazo vilivyowekwa katika miaka ya hivi karibuni.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.