Marekani yatishia kuendelea kuilenga Taliban ikiwa itaendelea na mashambulizi
Marekani inasema jeshi lake litaendelea kutekeleza mashambulizi ya angaa nchini Afghanistan kufuatia ongezeko la mashambulizi ya kundi la Taliban, wakati huu vikosi vya mwisho vikijiandaa kuondoka nchini humo ifikapo tarehe 11 mwezi Septemba mwaka huu.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Hata hivyo, jeshi la Marekani halijasema iwapo litaendelea kutekeleza mashambulizi hayo ya angaa baada ya kuondoka nchini humo.
Rais Biden alisema kuwa tarehe 31 mwezi Agosti ndio itakuwa “siku yetu ya mwisho hapa, baada ya siku hiyo tutaendelea kutoa misaada muhimu kwa jeshi la Afghanistan hasa, jeshi la angaa, kwa hivyo msaada huo utaendelea hata baada ya tarehe 31 mwezi Agosti.
Kumeshuhudiwa ongezeko la uasi kutokana na mashambulizi ya wanamgambo wa Taliban ambao pia wamedhibiti mipaka muhimu, wilaya kadhaa na kuizingira baadhi ya miji mikuu ya majimbo tangu mapema mwezi Mei, wakati muungano wa wanajeshi wa kigeni unaoongozwa na Marekani ulipoanza kuondoka nchini humo.
Taarifa ya wizara ya mambo ya ndani ya Afghanistan imesema "ili kukabiliana na machafuko na kuzuia vuguvugu la wanamgambo wa Taliban, kumeanzishwa zuio la watu kutotembea nje kwenye majimbo 31 nchini humo," kasoro Kabul, Panjshir na Nangarhar.Watu hawataruhusiwa kutembea kuanzia saa nne usiku hadi saa kumi za alfajiri kwa saa za nchini Afghanistan, amesema msemaji wa wizara hiyo ya mambo ya ndani Ahmad Zia Zia, kwenye taarifa ya sauti iliyosambazwa kwa waandishi wa habari.