Taharuki yatanda kwenye eneo la Jerusalem
Saa chache baada ya kutekwa na kisha kuuawa kwa mtoto mmoja raia wa Palestina, hali imezidi kuwa tete kwenye eneo la Jerusalem kufuatia makabiliano kati ya wanajeshi wa Israel na vijana wa Kipalestina.
Imechapishwa:
Tukio la kutekwa na kisha kuuawa kwa kijana wa Kipalestina linajiri wakati huu ambapo polisi nchini Israel wanaendelea na uchunguzi kuhusu tukio la kuuawa kwa vijana watatu raia wa Israel ambao walitekwa na kuuawa na kisha miili yao kitelekezwa kwenye msitu wa Jerusalem.
Hii leo kwa siku ya pili mfululizo, ndege za Israel zimeendelea na mashambulizi yake kwenye eneo la ukanda wa gaza hasa kwenye ngome za kundi la Hamas, ambalo Israel inadai ndilo limehusika na mauaji ya raia wake watatu.
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ametoa wito kwa pande zote mbili kutojiingiza kwenye mapigano wala vurugu wakati huu ambapo kumekuwa na hali ya sintofahamu kati ya raia wa Israel na Palestina.
Jumuiya ya kimataifa imelaani tukio la kuuawa kwa kijana wa Kipalestina na kuonya kuhusu kuendelea kushuhudiwa kwa matukio haya ya utekaji nyara ambayo inasema yanachochea kudhoofisha upatikanaji wa amani kati ya Israeli na Palestina.