Pata taarifa kuu
KENYA-SIASA-USALAMA

Rais wa zamani wa Kenya Daniel Arap Moi afariki dunia

Aliyekuwa rais wa pili wa nchi ya Kenya Daniel Torotich Arap Moi amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 95 baada ya kuumwa kwa muda mrefu.

Daniel Arap Moi, Rais wa zamani wa Kenya (kulia), hapa ilikuwa Disemba 28, 2002, muda mfupi kabla ya kuondoka madarakani.
Daniel Arap Moi, Rais wa zamani wa Kenya (kulia), hapa ilikuwa Disemba 28, 2002, muda mfupi kabla ya kuondoka madarakani. ALEXANDER JOE / AFP
Matangazo ya kibiashara

Tangazo hilo limetolewa na rais Uhuru Kenyatta leo Jumanne asubuhi. Kiongozi huyo wa zamani aliyeongoza Kenya kwa miaka 24, kabla ya kustaafu mwaka 2002, amekuwa akiumwa kwa muda wa kipindi kirefu, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 95.

Daniel Torotich Arap Moi, alikuwa rais aliyeongoza Kenya kwa muda mrefu katika historia ya nchi hiyo, kati ya mwaka 1978 hadi 2002.

Alichukua hatamu ya uongozi wa nchi kutoka kwa rais wa kwanza wa nchi hiyo Jomo Kenyatta baada ya kufariki dunia mwaka huo wa 1978, na atakumbukwa sana kwa umahiri wa kisiasa akiongoza chama tawala wakati huo cha Kanu.

Wakati wa uongozi wake, Moi, alipewa jina la Baba Moi, kwa sababu alipendwa na wananchi wa kawaida, hasa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kwa kuagiza wapewe maziwa mara kwa mara, yaliyofahamika kama maziwa ya Nyayo.

Hata hivyo, kwa mataifa ya Magharibi na wapinzani wake, aliongoza Kenya kwa mkono wa chuma, huku wakosoaji wake wakisema uongozi wake ulikiuka haki za binadamu na kuongezeka kwa kashfa za ufisadi.

Mwaka 1992, Moi alikubali mabadiliko ya katiba baada ya shinikizo, kutoka ndani na nje ya nchi hiyo na kukubali kuwepo kwa vyama vingi.

Hadi kifo chake, waliokosoa uongozi wake, wanamkumbuka kama kiongozi ambaye alikuwa dikteta aliyekataa kuondoka madarakani, lakini kwa waliompenda, wanamkumbuka kama kiongozi aliyehuburi amani na upendo na kuyasaidia mataifa jirani.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.