Pata taarifa kuu
UGANDA

Mtoto aliyeambukizwa Ebola Uganda afariki

Mtoto wa miaka mitano ambaye aliripotiwa kuwa na virusi vya Ebola nchini Uganda amefariki dunia, imesema taarifa ya wizara ya afya wakati huu hata wazazi wake wakiwa wamethibitishwa kuwa na virusi vya ugonjwa huo kutoka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Muuguzi Rachel Kahindo akiwa na mtoto ambaye anapatiwa matibabu ya Ebola Mashariki mwa DRC. Picha ya maktaba
Muuguzi Rachel Kahindo akiwa na mtoto ambaye anapatiwa matibabu ya Ebola Mashariki mwa DRC. Picha ya maktaba REUTERS/Baz Ratner/File Photo
Matangazo ya kibiashara

Shirika la afya duniani WHO limethibitisha kupitia ukurasa wake wa Twitter kuwa nchi ya Uganda imerekodi kesi tatu za Ebola, ikiwa ni maambukizi ya kwanza kuripotiwa nchini Uganda tangu ugonjwa huo uripotiwe nchini DRC.

Wizara ya afya ya Uganda hapo jana ilisema kuwa mwanamke mmoja mwenye asili ya DRC ambaye ameolewa na raia wa Uganda, walikuwa wameenda na mtoto wao pamoja na wanafamilia wengine wanne nchini DRC kumuhudumia baba yao ambaye baadae alifariki kutokana na Ebola.

Katika taarifa yake kupitia ukurasa wa kijamii wa Twitter, WHO inasema mtu aliyegundulika kuwa na virusi hivyo ni mtoto wa miaka 5 ambaye alikuwa anasafiri akitoka DRC na wazazi wake Juni 9 mwaka huu.

WHO imesema mtoto huyo na familia yake waliingia nchini Uganda kupitia mpaka wa Bwera ambapo punde baada ya kuingia waliomba kupata matibabu kwenye kituo cha afya na kuchukuliwa sampuli ya damu.

Wizara ya afya ya Uganda imethibitisha kuwepo kwa mgonjwa huyo ambapo imesema baada ya mtoto huyo kuchukuliwa sampuli ya damu, ilibainika kuwa na maambukizi ya virusi vya Ebola.

Tayari wizara ya afya nchini humo na WHO wametuma wataalamu wake kwenda kusaidia wataalamu walioko eneo la magharibi mwa Uganda kuwatibu na kutoa chanjo ya majaribio inayoendelea pia kutolewa mashariki mwa DRC.

Nchi ya Uganda imekuwa kwenye hali ya tahadhari tangu kuripotiwa kwa mlipuko wa virusi vya Ebola mashariki mwa DRC, ambako watu zaidi ya elfu 1 na 300 wameripotiwa kupoteza maisha.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.