Pata taarifa kuu
KENYA-BUNGE-SIASA-JINSIA-WANAWAKE

Wabunge nchini Kenya washindwa kupigia kura mswada muhimu

Wabunge nchini Kenya, wameshindwa kupigia kura mswada muhimu utakaowezesha idadi ya wanawake kuongezeka bungeni, kwa lengo la kutekeleza katiba ya mwaka 2010 kwa kikamilifu.

Bunge la Kenya, jijini Nairobi
Bunge la Kenya, jijini Nairobi www.parliament.go.ke
Matangazo ya kibiashara

Kiongozi wa walio wengi katika bungeni Adan Duale, amesema kuwa, idadi ya wabunge haikutosha, kuwezesha zoezi la upigaji kura kuendelea kama ilivyopangwa.

Kenya ina wabunge 349, na kwa mujibu wa kanuni za bunge hilo, kupigia kura marekebisho muhimu ya kipengele cha Katiba, wabunge 233 wanastahili kuwepo bungeni na kuupitisha kwa idadi hiyo.

Mswada huo sasa unatarajiwa kupigiwa kura mwezi Februari mwaka 2019.

Katiba ya mwaka 2010, iliweka wazi kuwa, nafasi za uteuzi katika mabunge hayo mawili, hazistahili kutawaliwa na jinsia moja, inayozidi thuluthi mbili.

Hata hivyo, Katiba hiyo haikueleza wazi namna ya kuepuka hali hiii, lakini Mwanasheria mkuu alikwenda katika Mahakama ya Juu, iliyoagiza bunge kurekebisha kifungu cha Katiba ili kutekeleza agizo hilo.

Mswada huo unabadilisha kifungu nambari 97 na 98 ili kuongeza idadi ya wanawake katika bunge hilo ambalo limetawaliwa na jinsia ya kiume katika historia ya siasa nchini humo.

Viongozi wa juu wa serikali, wakiongozwa na rais Uhuru Kenyatta, Naibu wake William Ruto na kiongozi wa upinzani Raila Odinga, wametoa wito kwa wabunge kuupitisha mswada huo ili kutoa nafasi kwa wanawake zaidi kuingia bungeni.

Kati ya wabunge 290 nchini Kenya, kwa sasa wabunge wanawake waliochaguliwa ni 22 na 50 wateule na kufanya idadi yao kufika 75. Iwapo mswada huu utapitisha idadi hiyo ya wanawake, inatarajiwa kuongezeka na kufikia zaidi ya 100.

Kenya ni ya mwisho katika ukanda wa Afrika Mashariki, kwa wanawake walio bungeni.

Rwanda ni ya kwanza kwa asilimia 61, Tanzania ni ya pili kwa asilimia 36 sawa na Burundi, huku Uganda ikiwa na asilimia 34 na Kenya ikiwa na asilimia 22.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.