Pata taarifa kuu
KENYA-SIASA-MARIDHIANO

Kenyatta na Odinga wakutana, wakubaliana kumaliza tofauti za kisiasa

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga, wamekutana kwa mara ya kwanza tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu uliopita na kuahidi kuliunganisha taifa hilo ambalo limegawanyika kisiasa.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta (Kushoto ) akisalimiana na kiongozi wa upinzani Raila Odinga baada ya kukutana Machi 09 2018 katika Ofisi ya rais jijini Nairobi
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta (Kushoto ) akisalimiana na kiongozi wa upinzani Raila Odinga baada ya kukutana Machi 09 2018 katika Ofisi ya rais jijini Nairobi twitter.com/UKenyatta
Matangazo ya kibiashara

Hatua hii haikutarajiwa na raia wa nchi hiyo huku viongozi hao wakisema watakuja na mpango wa kumaliza tofauti za kisiasa nchini humo na kukabiliana na ukabila.

Hata hivyo, Odinga na Kenyattta hawakueleza kwa kina ni mpango upi utachukuliwa ili kumaliza tofauti za kisiasa na kuhubiri maridhiano nchini humo.

“Tumekuja pamoja kuonesha kuwa nchi hii ni kubwa zaidi yetu, na ni lazima kwa wananchi wa nchi hii kuja pamoja,” alisema rais Kenyatta.

Naye Odinga, ambaye alikuwa ameapa kutomtambua rais Kenyatta kama kiongozi halali, amesema wakati umefika wa kumaliza tofauti za kisiasa kwa ajili ya nchi hiyo kupiga hatua.

“Katika kipindi cha historia ya nchi yetu, tumekuwa tukishughulikia siasa zetu ambazo zimetugawa kikabila na kidini na kwa bahati mbaya tumekuwa tukizikwepa,” alisema Odinga.

Mkutano huu umefanyika saa chache kabla ya kuwasili kwa Waziri wa Mambo ya nje Rex Tillerson jijini Nairobi.

Marekani imekuwa katika mstari wa mbele kushinikiza viongozi hao wawili kuja katika meza ya mazungumzo na kumaliza tofauti zao za kisiasa.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.