Pata taarifa kuu
KENYA-UCHAGUZI MKUU 2017

Kenya: Polisi yatawanya maandamano ya upinzani

Muungano wa upinzani nchini Kenya NASA umekashifu vikali matumizi ya nguvu dhidi ya wafuasi wake walioandamana hivi leo kwenye miji mbalimbali nchini humo ambapo polisi wametumia mabomu ya machozi kuwatawanya.

Polisi wa Kenya wakifyatua mabomu ya kutoa machozi dhidi ya waandamanaji wa upinzani. Jumanne, Octoba 24, 2017
Polisi wa Kenya wakifyatua mabomu ya kutoa machozi dhidi ya waandamanaji wa upinzani. Jumanne, Octoba 24, 2017 REUTERS/Thomas Mukoya
Matangazo ya kibiashara

Akizungumza na wanahabari hivi leo jijini Nairobi, wakili wa NASA James Orengo amesema kuwa muungano wao unasikitishwa na namna ambavyo polisi walishindwa kuheshimu amri ya mahakama na kuwatawanya wafuasi wake waliokuwa wakiandamana kwa amani.

Orengo amesema licha ya hapo jana kukutana na mabalozi wa Marekani na Uingereza na kuwahakikishia kuwa polisi hawatazuia maandamano yao, wameshangazwa namna ambavyo polisi walitumia nguvu kuwafurusha wafuasi wao.

Orengo amewakashifu vikali mabalozi wa nchi hizo akisema waliwadanganya kwa kuwapa hakikisho kuwa Serikali iliwahakikishia kuwa haitaingilia maandamano yao lakini hali ilikuwa kinyume.

NASA inasisitiza kuwa itaendelea mbele na maandamano yao hapo kesho licha ya kuwa wanafahamu fika polisi wataendelea kutumia mabavu kuzuia nguvu ya uma dhidi ya tume ya uchaguzi IEBC.

Katika hatua nyingine kinara wa NASA Raila Odinga ambaye amejiondoa kushiriki kwenye uchaguzi wa marudio wa juma hili, amekana kuwa aliwaamrisha wafuasi wake kuandamana siku ya kupiga kura na badala yake anasema alichowaambia ni kususia uchaguzi huo.

Hivi karibuni Raila Odinga alinukuliwa na vyombo vya habari vya ndani na vile vya kimataifa akiitisha maandamano makubwa siku ya Alhamisi.

Aidha kaimu waziri wa mambo ya ndani wa Kenya Fred Matian'g amesema siku ya Jumatano ya Octoba 25 itakuwa ni mapumziko kwa nchi nzima ili kutoa nafasi kwa raia wanaotaka kupiga kura kusafiri kwenda kwenye maeneo waliyojiandikisha.

Matian'g kwenye tangazo lake pia ametoa hakikisho kwa taifa kuwa usalama utaimarishwa kwenye maeneo yote ya nchi ili kuhakikisha watakaopiga kura wanashiriki kwa amani.

RFI Kiswahili imeshuhudia polisi wakirandaranda kwenye jiji la Nairobi na hasa kuzunguka ofisi za tume ya uchaguzi IEBC, huku watu waliojaribu kuandamana kuelekea kwenye ofisi hizo wakifurushwa na vitoa machozi.

Licha ya maandamano yaliyotangazwa na NASA, hivi leo shughuli zimeendelea kama kawaida katikati mwa jiji la Nairobi licha ya kuwa baadhi ya maduka yamefungwa kwa hofu za maandamano.

Mwandishi wetu Emmanuel Makundi aliyeko Nairobi anasema ameshuhudia ulinzi wa hali ya juu kwenye maeneo mengi ya jiji huku kwenye baadhi ya sehemu baadhi ya wakina mama wakiruhusiwa kufanya maandamano ya amani.

 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.