Pata taarifa kuu
KENYA-HAKI ZA BINADAMU

Tume isiyo ya kiserikali ya kutetea haki za Binadamu nchini Kenya, yasema inatishwa

Tume isiyo ya kiserikali ya kutetea haki za binadamu nchini Kenya, KHRC, imelaani hatua ya Bodi inayosimamia Mashirika yasiyo ya kiserikali nchini humo  kwa kuipokonya leseni ya kuendelea na shughuli zake.

Mwenyekiti wa Tume hiyo George Kegoro akizungumza na wanahabari siku ya Jumanne, Agosti 15 2017
Mwenyekiti wa Tume hiyo George Kegoro akizungumza na wanahabari siku ya Jumanne, Agosti 15 2017 /twitter.com/thekhrc?
Matangazo ya kibiashara

Siku ya Jumatatu, Mkurugenzi wa bodi hiyo Fazul Mahamed, alituma taarifa katika vyombo vya Habari kuifuta Tume hiyo kwa madai kuwa imekuwa ikikwepa kulipa kodi na haijaeleza chanzo cha mapato yao lakini pia kuwaajiri watalaam kutoka nje bila ya kuwatafutia vibali vya kufanya kazi.

Mwenyekiti wa Shirika hilo, George Kegoro, amesema Bodi hiyo inaitisha kisiasa kutokana na harakati zake za kuikosoa serikali mara kwa mara na kuongeza kuwa madai haya, yamewahi kupinga Mahakamani na kinachoendelea ni ukiukwaji wa haki zao kikatiba.

Aidha, Kegoro amesema hawajapata barua yoyote rasmi ya kufutwa kwao kama inavyoripotiwa katika vyombo vya Habari nchini humo.

“Hajawahi kutuandikia barua, kutoa malalamishi yake, hana mawasiliano mazuri nasi, ameendelea kutulenga kwa sababu anahisi kuwa tunaikosoa serikali,” amesema George Kegoro.

“Hana mamlaka na uwezo wa kutufuta na kuingilia kazi zetu, na madai dhidi yetu hayana msingi wowote,” ameongeza Kegoro.

Wakati uo huo, Bodi hiyo imetaka kufutwa kwa Shirika lingine lisilo la kiserikali la AfriCOG, kwa madai kuwa inaendeleza shughuli zake kinyume na sheria.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi huyo Fazul Mahamed ameiandikia barua Ofisi ya makosa ya jinai kutaka kukamatwa kwa viongozi wake.

Fazul ameitaka Benki Kuu kuzuia, fedha za Shirika hilo na kuzuia mali zake.

Mashirika tya kutetea haki za binadamu na wanaharakati, wamelaani hatua hii. KHRC na AfriCOG, yameendelea kulaani mauaji ya polisi dhidi ya mauaji ya waandamanaji lakini pia imekuwa ikihoji uhalali wa rais Uhuru Kenyatta.

Hatua hii pia imelaaniwa na Kanisa Anglikana nchini humo.

Askofu wa Kanisa hilo Jackson Ole Sapit ameitaka serikali kuyaacha mashirika hayo kuendelea na kazi zao.

Aidha, ametaka kuundwa kwa Tume maalum, kuchunguza namna Uchaguzi Mkuu ulivyofanyika hasa, ule wa urais.

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga, amekataa kutambua ushindi wa rais Uhuru Kenyatta na kusema kuwa yeye ndiye aliyeshinda Uchaguzi huo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.