Pata taarifa kuu
KENYA-SIASA-UCHAGUZI

Meneja wa Teknolojia katika Tume ya Uchaguzi nchini Kenya auawa

Meneja wa Teknolojia  katika Tume ya Uchaguzi nchini Kenya Chris Musando, amepatikana ameuawa baada ya kutoweka kuanzia Ijumaa, wiki iliyopita.

Marehemu Chris Musando akizungumza katika mikutano iliyopita na wanahabari jijini Nairobi kabla ya kutoweka kwake.
Marehemu Chris Musando akizungumza katika mikutano iliyopita na wanahabari jijini Nairobi kabla ya kutoweka kwake. reutersmedia.ne
Matangazo ya kibiashara

Polisi wanasema mwili wa Musando aliyetoweka siku ya Ijumaa, ulipatikana katika eneo la Kikuyu katika nje kidogo ya jiji la Nairobi.

Mwili wa afisa huyo wa IEBC pia ulipatikana pamoja na wa mwanamke mmoja ambaye hajafahamika.

Kupatikana kwa mwili wa Musando kumezua hali ya wasiwasi kwa maafisa wa Tume ya Uchaguzi, ambao walikwenda katika chumba cha kuhifadhi maiti cha City jijini Nairobi kuangalia mwili wake.

Vyombo vya Habari nchini Kenya vinaripoti kuwa, maafisa wa chumba hicho cha kuhifadhi maiti, wamesema mwili wa Musando ulikuwa na alama za majeruhi  ishara kuwa aliteswa kabla ya kupigwa risasi.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Wafula Chebukati amesema wameshangazwa na mauaji hayo na kuongeza kuwa, hakuna shaka kuwa Chris Musando aliuawa.

Aidha, ametaka maafisa na wafanyikazi wote wa Tume ya Uchaguzi kupewa usalama wa kutosha kipindi hiki nchi hiyo ikijiandaa kuwa na  Uchaguzi.

"Tunataka kufahamu ni nani na kwanini walimuua Chris Musando," amesema Chebukati.

Wachambuzi wa siasa na usalama nchini humo wanahoji, ni vipi afisa huyo muhimu alikosa usalama lakini pia mazingira ya kutoweka kwake.

Maswali mengi yanaulizwa kuhusu kuuawa kwa Msando ambaye imebainika kuwa aliuuawa Jumamosi lakini taarifa zake zimefahamika siku ya Jumatatu.

Kabla ya kupatikana kwa mwili wake, gari lake lilipatikana pembezoni mwa barabara Kuu ya Thika na kupelekwa katika kituo cha Polisi mtaani Kasarani.

Kuna hofu kuwa, afisa huyo wa IEBC aliuawa mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kutoweka katika mazingira ya kutatanisha.

Musando amepatikana ameuawa siku ambayo alitarajia kuongoza majaribio ya mitambo ya  teknolojia, kuelekea Uchaguzi wa Jumanne ijayo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.