Pata taarifa kuu
KENYA-SIASA-UCHAGUZI

Odinga ajitokeza kwenye mdahalo, Kenyatta aukwepa

Mgombea mkuu wa upinzani nchini Kenya kupitia muungano wa upinzani NASA Raila Odinga, alitumia dakika 90 katika mdahalo wa wagombea urais Jumatatu usiku kueleza sera zake, kwa wananchi wa nchi hiyo ikiwa atashinda Uchaguzi Mkuu wa mwezi ujao.

Mgombea wa muungano wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga, akiwa kwenye mdahalo wa wagombea urais siku ya Jumatatu Julai 24 2017
Mgombea wa muungano wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga, akiwa kwenye mdahalo wa wagombea urais siku ya Jumatatu Julai 24 2017 REUTERS/Thomas Mukoya
Matangazo ya kibiashara

Odinga alitarajiwa kupambana na rais Uhuru Kenyatta katika mdahalo huo lakini hakujitokeza na kumwacha Odinga peke yake jukwani kujibu maswali mbalimbali.

Waziri huyo Mkuu wa zamani, alisema alitamani sana rais Kenyatta angekuwepo katika mdahalo huo ili amuulize maswali na kupambana naye kwa hoja lakini ni bahati mbaya hakuwepo.

“Nilitamani sana rais Kenyatta angekuwa hapa, nimuulize maswali wazi wazi lakini amenichezea shere,” alisema Odinga.

“Namtakia kila la heri yeye na rafiki yake Ruto, katika uchaguzi huu ambao utakuwa kama mchuano wa kirafiki, na asiyekubali kushindwa sio mshindani,” aliongeza.

Miongoni mwa ahadi ambazo Odinga alidokeza kuwa serikali yake itashughulikia ni pamoja na kushughulikia changamoto ya ajira, kupunguza gharama ya maisha na kodi ya nyumba.

Kuhusu madai kuwa muungano huo una kituo cha kujumuisha matokeo nchini Tanzania, Odinga aliyakanusha na kusema kituo chao kipo nchini Kenya.

“Kwanini kuna hofu kuhusu haua yetu na kuwa na kituo cha kujumuisha matokeo, ikiwa kipo Ujerumani, Marekani au kwenye mwezi ?, “ aliuliza Raila.

“Kituo chetu kipo hapa nchini Kenya, Kenya na kwenye mawingu,” aliongeza.

Soma hii pia.Bonyeza.

Wachambuzi wa siasa nchini Kenya, wamekosoa hatua ya rais Kenyatta kutokwenda katika mdahalo huo kwa kile wanachosema alikosa nafasi ya kujieleza.

Aidha, wamedokeza kuwa Odinga alionekana kufahamu mambo mengi sana yanayoikumba nchi hiyo kutokana na uzoefu wake wa muda mrefu kama kiongozi wa kisiasa nchini humo lakini pia Waziri Mkuu.

Kampeni ya rais Kenyatta ilidokeza kuwa hakushiriki katika mdahalo huo kwa sababu hakuridhika na maandalizi na mpangilio wa mdahalo huo.

Wagombea wengine watatu Ekuru Aukot, Japhet Kavinga na Profesa Michael Wainaina nao walishiriki katika mdahalo huo ulioandaliwa mapema kuanzia saa kumi na moja na nusu.

Hata hivyo, mdahalo huo ulisusiwa na wagombea wengine watatu Joe Nyagah, Cyrus Jirongo na Abduba Dida.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.